RAIS SAMIA AFUNGUKA KUMBUKIZI MWAKA MMOJA KIFO CHA MAGUFULI

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini kitabu cha kumbukumbu kabla ya kuweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kufariki dunia kwa Hayati Dkt. Magufuli leo tarehe 17 Machi, 2022. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Michezo wa Magufuli leo tarehe 17 Machi, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimfariji Mama Janeth Magufuli baada ya kuweka Shada la Maua katika Kaburi la Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Michezo wa Magufuli leo tarehe 17 Machi, 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Wananchi wa Chato pamoja na Wageni kutoka Sehemu mbalimbali nchini katika Kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu kufariki dunia kwa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa Michezo wa Magufuli leo tarehe 17 Machi, 2022. 

**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,amefunguka kuhusu mtanziko wa fikra aliopata juu ya madaraka anayokaimishwa kwa kujiuliza atakapoanzia kuongoza Taifa na kwamba hofu yake ilipata jibu alipokumbuka aanzie alipokomea mtangulizi wake.

Rais Samia ameyasema hayo leo Alhamisi, Machi 17, 2022 wakati akitoa salamu za taifa katika maadhimisho ya mwaka mmoja wa kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya 5 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Viwanja vya Magufuli, Chato mkoani Geita.

"Kwangu ilikuwa ni siku ya mshtuko na tafakuri juu ya dhamana inayotwishwa mabegani kwangu bila kujiandaa, nikiri swali kubwa kwangu lilikuwa hivi ninaanzia wapi, baada ya muda nikajisemesha moyoni kwamba nitaanzia pale Kaka yangu alipoishia," amesema Rais Samia akiwaongoza Watanzania kumkumbuka na kumuenzi kiongozi huyo shujaa.

"Machi 17 2021 ilikuwa ni siku ngumu ya huzuni na simanzi kubwa kwa familia ya Hayati Magufuli, wingu kubwa la hofu lilitanda nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla, watu wakitafakari kuondokewa na uongozi uliokuwa na weledi na uzalendo", ameeleza Rais Samia.

Amesema Dkt. Magufuli alikuwa mzalendo aliyependa kuliona Taifa linanyanyuka kiuchumi huku akipiga Vita rushwa na ubadhirifu wa Mali za umma,hivyo alirejea kauli yake kuendeleza miradi aliyoacha mtangulizi wake na kutekeleza mipya kwa maslahi ya Taifa.

"Hivi karibuni tutafungua daraja la Tanzanite lililopo jijini Dar es salaam hii ilikuwa ndoto ya Magufuli na nitaiendeleza kwa kuboresha huduma za maji, umeme na miundombinu. Kwa upande wa mradi wa kivuko cha Chato-Nkome kilichogharimu Shilingi Bilioni 3.1 umekamilika na Mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi unaojengwa kwa Shilingi Bilioni 13.2 umekamilika kwa asilimia 92. Tutaendelea kutoa fedha ili ukamilike kwa asilimia 100",amesema Rais Samia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments