WIZARA YA NCHI OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA YAELEZA MAFANIKIO MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais utumishi Jenista Mhagama akiongea na wandishi wa habari leo Dodoma kuhusu mafanikio ya wizara yake ikiwa ni  mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

KWA kipindi cha mkwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesema imefanikiwa kuanza kujenga Mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) ili kuondokana na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama wakati akiongea na Waandishi wa habari na kuongeza kuwa amesema mfumo huo wa Public Employees  Management Information System (PEPMIS) utakuwa ni wa kielektroniki na utaondokana na matumizi ya makaratasi.

“Pia utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji wa watumishi,lakini pia utaweka mifumo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi wa watumishi kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa na yanayopimika”,alisema Mhagama.

Pia alisema kuwa mfumo huu pia utahamasisha uwajibikaji wa hiari na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa watumishi.

Wakati huo huo alisema kuwa katika kipindi hiki Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi Public Institutions Performance Management Information System (PIPMIS).

“Mfumo huu ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja”,alisema.

Alisema kuwa makubaliano hayo yatakuwa kati ya viongozi wakuu wa taasisi na viongozi wao wanaowasimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa kila siku. 

“ Utekelezaji wa mfumo wa huu wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na taifa kwa ujumla, kuimarisha utamaduni unaojali matokeo, na kuleta matumizi bora ya rasilimali za umma”,alisema. 

Wakati huo huo amesema kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kujenga Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI kwa lengo la kuwawezesha watumishi na wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi na Utawala.

Amesema mfumo huo unampa fursa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kufuatilia namna masuala ya utumishi na Utawala Bora yaliyowasilishwa na wananchi na watumishi wa Umma yalivyofanyiwa kazi na kumuwezesha Waziri kufuatilia hali ya uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utumishi na utawala bora.

“Mfumo huu pia unamuwezesha Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kuongea moja kwa moja na mlalamikaji ili kujua ni kwa namna gani tatizo lake limefanyiwa kazi na kuchukua hatua stahiki”,amesema. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments