WANAKIJIJI BUTIAMA WAKACHA KUCHOTA MAJI YA BOMBA WADAI SH. 50 NI PESA NYINGI

Mwananchi wa kijiji cha Masurura akichota maji yasiyo safi na salama
Mashine yakusukuma maji kijiji cha Masurura


Na Dinna Maningo,Butiama

Ugumu wa Maisha unatajwa kuwa ni moja ya sababu inayosababisha baadhi ya wananchi katika kijiji cha Masurura kata ya Bwirege wilaya ya Butiama mkoani Mara,kuacha kuchota maji ya bomba na kuendelea kuchota maji katika visima vya asili na mito ambayo siyo safi na salama kwa kile walichoeleza kuwa malipo ya shilingi 50 kwa ndoo moja ya maji ni pesa nyingi nakwamba wao wamezoea kuchota maji bila malipo.


Licha ya Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutoa fedha za kujenga,kukarabati na kupanua miradi ya maji katika wilaya hiyo kama njia ya kupunguza tatizo la ukosefu wa maji safi na salama vijijini,bado wananchi wanatumia maji yasiyo salama huku wengine wakidai tatizo ni ukosefu wa elimu juu ya umuhimu wa kutumia maji safi na salama.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kutembela miradi ya maji katika wilaya hiyo,mkazi wa kijiji hicho Ester John alisema "Watu wanakwepa kuchota maji ya bomba kwasababu ya gharama sh.50 kwa maisha ya hapa kijijini kwetu ni pesa nyingi,ardhi yetu yenyewe ni changamoto hata kupata mazao ya uhakika uuze upate pesa ni shida.

“Sisi tunategemea kilimo ukivuna mazao ukauze ili upate pesa ya kununua mboga na mahitaji mengine bado tena ununue maji na kwa maisha ya kijijini kuna familia zina watu 10 kwa siku wanatumia maji mengi hata zaidi ya ndoo 10 kila siku hiyo 500 itatoka wapi ?na haya maisha yetu ya kijijini tunayoishi kwa kutegemea kilimo kwakuwa hatuna pesa tunatumia maji ya visima kwakuwa yenyewe tunachota bure bila malipo”,alisema Ester.


Raheli Mugesi alisema "Pesa yakununua mafuta ya kula,nyanya au vitunguu ili uunge mboga hakuna tunakula mboga chukuchuku hiyo pesa ya kulipa kila siku inatoka wapi?tunakunywa uji hauna sukari siyo kwamba tunapenda hapana!nikwasababu ya ugumu wa maisha na pesa kuipata ni kazi hakuna biashara huku zakutuingizia fedha alafu wanatuuzia maji!.

"Kwani ni biashara?hii ni huduma hatukupaswa kutozwa tena fedha ,serikali kama imeamua kutusaidia wananchi wa vijijini tupate maji bure au tulipe kwa mwezi sh.2,000 kama tunavyolipa kwenye visima vya watu wengine vinginevyo maji ya bomba watakuwa wanatuona wakati wa kiangazi visima vinapokauka’’,alisema Mugesi.

Bhoke Wambura alisema "Maisha ya watu wa vijijini ni magumu siyo kama watu wanaoishi mjini ambako kuna fursa nyingi zakutafuta pesa,tunafurahi kutupatia mradi unatusaidia hasa wakati wa kiangazi lakini tatizo bado halitaisha kama watu wataendelea kutumia maji yasiyo safi na salama kwasababu ya fedha.


"Watu wakiacha kuchota maji mradi hautakuwa na tija ukizingatia mradi wenyewe jamii ndiyo inauendesha kifaa kikiharibika fedha za maji ndiyo zitengeneze licha yakwamba mjini matengenezo ya mradi yanasimamiwa na MUWASA na ajira wanalipa wao lakini sisi huku vijijini wanategemea makusanyo ya pesa za maji ndiyo watu walipwe asilimia 10’’,alisema Bhoke.


Naomi Juma alieleza "Yaani nitoe pesa kuchota maji bombani wakati kuna maji ya bure kisimani! maji yenyewe mpaka upange foleni wakati kisimani ukifika unachota maji unaondoka zako bombani mpaka usubiri zamu kituo kimoja cha maji wanachota kitongoji kizima inasababisha watu wachote kisimani kwa sababu yak uogopa foleni,foleni kubwa wakati mwingine watu wanapigana wanagombania maji mwenye nguvu ndiyo anachota haraka”,alisema Naomi.

Maseke Marato alisema kuwa watu wanachota maji visimani ili kuepuka gharama "Watu wanatumia maji ya visima na mto kwa kufua,kuosha vyombo,kunywesha mifugo ili kuepuka gharama anayetumia maji machafu ni kwa sababu ya ugumu wa maisha pesa inakosa hata ya kununua kiberiti,bombani wanaenda tu kufuata maji ya kunywa.

"Awali huu mradi ulikuwa unaendeshwa kwa mafuta ya dizeli na tulichota bure bila kulipia sema kulikuwa na changamoto ya maji tulikaa hata miezi mitatu bila kupata maji ya bomba kwasababu mashine ilikuwa inafanya kazi mara chache yakitoka yanakaa muda ndiyo yatoke,tulichota maji machafu,ila baada ya mradi huu kurekebishwa mashine inaendeshwa kwa umeme’’,alisema.

Maseke alisema kuwa watu hawana uelewa wa umuhimu wa kutumia maji safi na salama nakwamba wakihamashishwa na kupewa elimu itawasaidia kutoendelea kutumia maji machafu"kinachohitajika ni elimu kuna watu watoto wao hawavai nguo utawaona matumbo wazi lakini nguo zipo sh.1000 hawanunui watoto wanakaa uchi,unakataa kutoa sh. 50 unatumia maji machafu ukiugua unatibiwa kwa zaidi ya 20,000 yote ni kwasababu tu ya uelewa mdogo watu waelimishwe’’alisema.

Elizabeth William mkazi wa kitongoji cha senta alisema kuwa mradi huo wa maji umewasaidia na kwamba kabla ya mradi huo walichota maji kwenye malambo ambayo si safi na salama hivyo watu kukwepa maji ya bomba na kwenda kwenye visima ambavyo baadhi maji siyo safi ni kutokana na uelewa mdogo wa umuhimu wa kutumia maji safi na salama.

Josephu Mugendi alisema kuwa mradi huo umesaidia kupunguza wimbi la watu kutumia maji yasiyo safi na salama kwakuwa yanapatikana bombani lakini aliiomba RUWASA kuhakikisha inasambaza maji katika vitongoji vyote na kuhakikisha maji hayakatiki kwakuwa wakati mwingine maji hukosa kwa siku tatu.

Mwenyekiti wa kamati ya Jumuiya ya watumiaji wa maji Masurura (CBUSO) Jacob Hezekia, alisema kuwa kitendo cha wananchi kukwepa kuchota maji ni mazoea na jambo hilo linarudisha nyuma mapato yatokanayo na mradi "mradi ukishakamilika unakabidhiwa kwa wananchi kuusimamia na kuuendesha kifaa kikiharibika fedha za maji ndiyo tunachukua na kurekebisha na pesa hizo hizo bado tumlipe mlinzi na mhasibu hazitoshi.


‘’Mradi ulianza 1981 uliendeshwa kwa mafuta ya dizeli wakati huo wananchi walichota maji bure ,tangu mwaka jana mashine inatumia umeme watu wanalipa sh. 50 kwa ndoo moja fedha ambazo ni kwa ajili ya uendeshaji wa mradi.

"Bomba zinapasuka ovyo,ili kuzuia chngamoto ya wizi wa maji chemba za DP ziwekewe mifuniko ya bati ili tufunge kufuri kuzuia wizi wa maji lakini hizi ni za zege watu wanatoa na kuchota maji,tuna DP 20(vituo vya kutoa huduma ya maji) zinazofanya kazi ni DP 18 moja bado haijakamilika ni nyingine tuliifunga baada ya kukosa msimamizi”,alisema.

Jacob alisema kuwa hadi sasa kuna makusanyo ya fedha za maji sh.135,000 zilizopo benki "fedha zinazopatikana ndiyo zinatumika kwenye matengenezo ya mradi,tunalipa umeme na tunamlipa mlinzi,Mhasibu na katibu asilimia 10 ya malipo ya maji,kuna shida ya getivalvu hakuna bomba likiharibika maji yanamwagika hakuna namna ya kuyazuia inabidi ufunge tenki au laini ya maji iliyopasuka.

Alisema kuwa baadhi ya wananchi hawajafikiwa na mradi wa maji wakiwemo wa kitongoji cha Bumagwa,Sei,Malama,Nyakangara,Taho na Kumunya wanatembea umbali zaidi ya km 3 kutafuta maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini( RUWASA)wilaya ya Butiama,Mafuru Dominico alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha kutekeleza miradi saba ya maji kiasi cha Bilioni 2.4,vijiji vilivyonufaika na miradi ya maji ni kijiji cha Biatika kata ya Buhemba,Nyasirori kata ya Masaba.

Aliongeza kuwa miradi mingine ni ya fedha za UVIKO-19 kijiji cha Nyamikoma kata ya Kyenyari,kijiji cha Mwibagi kata ya Kyenyari,Buswahili kata ya Buswahili,Kyankoma kata ya Nyamimange na mradi wa uboreshaji wa visima vya pampu ya mikono kwa kufunga sora za umeme katika vijiji vinne ambavyo ni kijiji cha Mmazami,Kyatungwe,Masurura na Nyambili na itakamilika juni 30/2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post