WAZIRI MKENDA ATAKA TAEC KUTOA HAMASA KWA WANAFUNZI KUPENDA MASOMO YA SAYANSI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiongea mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Ofisi za TAEC Kikombo jijini Dodoma.
Mkurungenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala akifafanua jambo wakati wa uwekaji  jiwe la msingi ambapo ameeleza kuwa Serikali kupitia tume hiyo  imeweka mikakati ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga Ofisi hiyo ambayo itakuwa na maabara tano za sampuli za vyakula, mazingira,tathimini ya viwango vya mionzi kwa wafanyakazi na kuwaepusha na madhara,maabara ya matengenezo ya vifaa vya nyuklia ,maabara ya sampul za mazingira,maabara ya ulinzi na usalama wa kinyukilia .

***

 Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.

WAZIRI wa Elimu Sayansi  na Teknolojia  Profesa Adolf Mkenda ameweka  jiwe la msingi la maabara na Ofisi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)Kikombo jijini Dodoma huku akiitaka tume hiyo  kuwajengea uwezo na kuwapa hamasa wanafunzi wa kitanzania kusomea masomo ya sayansi ili kuwa na wanasayansi wengi kwa uchumi wa nchi.

Akiongea mara baada ya kuweka jiwe la msingi jana,Prof.Mkenda amesema kuwepo kwa Ofisi hizo Jijini Dodoma kutatoa fursa kwa wanafunzi mbalimbali kufika ili kujifunza jinsi ambavyo wanaweza kupata manufaa ya uwepo wa tume hiyo na kujifunza kwa vitendo wanayosoma darasani.

Amesema,hatua hiyo itaongeza juhudi za kuwaandaa Wanasayansi wa kutosha na kwamba ipo haja ya wizara hiyo  kuhakikisha vijana waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi wanapata ufadhili wa kusoma Vyuo vikuu nje ya Nchi.

Ameeleza mkakati wa Serikali kuwa ni kuhakikisha vijana waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi wanapata ufadhili (schoolaship) kwenye masomo yao ili  wawe wajuzi na wabobezi.

"Kwa sasa tumepiga hatua kubwa ,ujenzi huu ukikamilika utakuwa na manufaa kwa jamii mzima,Kwa wanafunzi  baadhi ya mashine walikuwa wanazisoma darasani tu, lakini jambo la kufurahisha wataziona kwa macho yao na kuonyeshwa kwa vitendo na jinsi zinavyoweza kufanya kazi na kuleta tija kwa Taifa ,

Tunahitaji  Wanasayansi  tuna jukumu la kusomesha Watanzania  masuala ya nguvu za Atomiki hivyo nawaomba TAEC kutenga fedha ili Wanafunzi bora Kabisa wa sayansi wapate ufadhili,tukitenga fedha kila mwaka watakuwa wakienda kusoma nchi nyingi zilizoendelea  kisayansi,"amefafanua.

Amesema nchi inahitaji vijana wabobezi wa Sayansi na Teknolojia ili watumike kukuza uchumi na kwamba kwa kutambua umuhimu huo  kuna mkakati wa kukutana na Watanzania wanaofundisha Vyuo vikuu vya nje ili wafungue milango na kuona ni kwa jinsi gani vijana wa Tanzania watapata ufadhili.

"Tunao watanzania wengi wanaofundisha Vyuo vikuu nje ya Nchi, tutakaa nao ,watatufungulia milango  kuona namna gani tutawezesha vijana wetu,pia tuna mkakati mwingine wa  kuongea na balozi mbalimbali kuhusu vijana wanaofaulu vizuri masomo ya Sayansi wapate ufadhili ambapo pia Serikali nayo itakuwa na mchango wake katika kufanikisha jambo hilo,"amesema Waziri Mkenda.

Aidha, Waziri Mkenda ameipongeza TAEC kwa kuwa na maarifa ya kuwezesha  kupima kiwango cha mionzi katika vyakula kutoka nje ya nchi Kwa kushirikiana vyema na taasisi mbalimbali za Serikali hususani Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) kujua kama muhusika ana kibali na kuhakikisha kwamba watanzania na wananchi hawapati madhara.

Kutokana na hayo Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambichaka amesema  wanatazamia kuanzisha ufadhili (schoolaship)  kwa wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya Sayansi kwenda kusomea Teknolojia ya nyuklia kwa matumizi salama ya mionzi na kuendeleza teknolojia ya nyukilia .

"Tunategemea kuanzisha mafunzo katika Sayansi ya nyuklia kwa kutumia wataalam waliopo ATEC,tunaomba pia  kuangaliwa kwa suala la kuondoa tozo ambazo si za lazima katika mionzi,"amesema.

"TAEC inajivunia kwa uwezo wanaojengewa na Serikali ambao umeifanya kuwa ni tume pekee kwa upande wa Afrika ya Mashariki na kati yenye mitambo ya kisasa ambayo husaidia sana wananchi kuwa salama na ukizingatia kwamba shughuli nyingi za Serikali hutegemea mionzi hiyo ya asili na ya kutengeneza,"amesema.

Naye Mkurungenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala amesema Serikali kupitia TAEC imeweka mikakati ya kusogeza huduma karibu na wananchi Kwa kujenga Ofisi hiyo ambayo itakuwa na maabara tano za sampuli za vyakula, mazingira,tathimini ya viwango vya mionzi kwa wafanyakazi na kuwaepusha na madhara,maabara ya matengenezo ya vifaa vya nyuklia ,maabara ya sampul za mazingira,maabara ya ulinzi na usalama wa kinyukilia .

Amesema ujenzi huo Wenye eneo la mita  za mraba 1602 hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi bilioni 3.8  gharama hizo ni pamoja na kuweka mandhari nzuri na uzio.

"Jengo hili litakuwa na Ofisi 27 kwa kuhusisha chumba cha mkutano pamoja na sehemu maalumu ya kufanya mazoezi Kwa wafanyakazi ilikuwasaidia kujenga afya,lengo ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanaofanya kazi katika sekta hii hawadhuriki,"amesema

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments