KATIBU UVCCM TAIFA AWATAKA VIJANA KUACHA MAJUNGU,ASEMA RAIS SAMIA ATAONGOZA HADI 2030

Katibu UVCCM Taifa,Kenani Kihongosi na viongozi wengine na vijana wa UVCCM wakitembelea miradi Tarime

****
Na Dinna Maningo, Tarime

KATIBU wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Kenani Kihongosi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu ataongoza hadi 2030 kwa kuwa ndiyo utaratibu wa chama Rais kuongoza katika kipindi cha miaka kumi na kwamba asiyetaka aende zake.

Kihongosi aliyasema hayo jana kwenye kikao cha UVCCM kilichofanyika Kitaifa katika Hoteli ya CMG mjini Tarime,wakati wa kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa CCM na kukumbushana mambo ya chama kilichohudhuriwa na wanachama wa Umoja huo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.


Washiriki wengine ni baadhi ya viongozi wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tarime Daud Ngicho,Mbunge wa jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki, Mwita Waitara Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Tarime Daniel Komote na Simon Samwel wa halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Katibu huyo wa UVCCM Taifa alisema kuwa Chama cha CCM siyo chama cha mtu kusema anavyotaka kwani kina taratibu zake,kanuni,miongozo na katiba na kwamba kwa yeyote atakayemuongea vibaya Rais Samia UVCCM wataruka nae.


"Wapo watu wanamuongea Rais wanavyotaka,sisi vijana hatutakubali mtu ndani ya chama anakichafua chama na Rais, asiyemtaka aende zake huko,kama mtu akija vibaya tutaruka nae,wajibu wetu ni kumlinda Rais wetu na chama chetu,2025 tunachukua tunaweka waaa" alisema Kihongosi.


Katibu huyo aliwataka vijana wa UVCCM kuacha chuki,uongo,umbea na kujipendekeza kwa madai kuwa inashusha heshima na kwamba malumbano kisa cheo siyo vizuri na badala yake washirikiane.


"Watu wanajipendekeza hadi inakera,tuache majungu,watu wanatengeneza maneno ya uongo, umbea,wengine wanapiga simu kwa viongozi wanaongea mambo ya ovyo ovyo mambo ya uongo ambayo hayapo ilmradi kumshusha mtu,jambo la kijana mwenzetu ni letu sote,tuache tabia za umbea,uchonganishi na kujipendekeza" alisema.


Kiongozi huyo alisema UVCCM wakishirikiana watafika mbali huku akiwasisitiza vijana kutovunja undugu kisa madaraka kwani mbali na uongozi wao ni familia moja wana wajibu wa kushirikiana kwakuwa Rais Samia ameonesha imani kubwa hivyo wasimuangushe.


Akizungumzia uchaguzi ndani ya chama hicho aliwaomba vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na siyo kubeba mikoba ya viongozi huku akikemea tabia ya baadhi ya wanachama wanapoona vijana wakionesha nia ya kugombea wanawaridisha nyuma.


"Tuache vijana wajitokeze kugombea hii tabia ya kuona kijana anaonesha nia unamrudisha nyuma hili jambo sitalikubali,nawapongeza vijana wa Tarime mnajituma jambo langu moja, Tarime chapeni kazi,niwapongeze viongozi wote wa chama mkoa na wilaya mmetupokea vizuri na mmefanya kazi nzuri,nimpongeze Dc Rorya ni kijana nilikuwa Rorya tumeona kazi zake nzuri" alisema.


Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar,Mussa Haji alisema kuwa wamefurahi Baraza la la UVCCM Taifa kufanyika wilayani Tarime nakuwapongeza kwa ukaribu wao na akaomba wakati ujao Baraza hilo lifanyike Zanzibar.


Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Mara Jacob Mangaraya aliwataka waliovuka umri wa ujana wa miaka 35 kuwaachia wengine nafasi kwa madai kuwa baadhi ya watu ung'ang'ania nafasi hiyo licha ya kuvuka umri "Tunalipongeza Baraza la kuu la UVCCM kwa upendo wenu wa kuja Mara wilaya ya Tarime kuzungumza na vijana,niwaombe viongozi tuliovuka umri wa vijana tuachie wengine nafasi" alisema.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime Daud Ngicho aliwahimiza vijana kuzingatia maadili na heshima na pale wanapoonywa au kukosolewa kutofanya jambo ambalo ni kinyume wawe tayari kusikiliza na kuwa tayari kutii.


Aliongeza kuwa Tarime haina ukabila kwani wapo viongozi ndani ya chama ndani ya wilaya hiyo si Wakurya akitolea mfano kwa Mwenyekiti wa UVCCM wilaya Godfrey Francis ambaye ni mkazi wa Tarime na mwenyeji kutoka wilaya ya Rorya pamoja na Katibu Hamasa wilaya hiyo Remmy Mkapa anayetoka mkoa wa Singida.


Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara alipongeza UVCCM kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM Kitaifa katika wilaya ya Tarime na kusema kuwa shughuli nyingi alijifunza wakati alipokuwa UVCCM.


Mbunge wa jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki yeye aliisifia wilaya hiyo na kuwakaribisha tena vijana kwa kuwa Tarime hakuna njaa vyakula ni vingi na ardhi ya Tarime ina rutuba nzuri inayostawisha mazao.


Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka alisema"Mimi niliposikia vijana wanakusanyika Tarime nilisema lazima nifike kwa namna yoyote ile nimelelewa na kukuzwa UVCCM nipo Rorya kimwili lakini kiroho nipo pamoja na nanyi,hakuna kitu kikubwa kama kuweka alama kwa watu unaoishi nao lazima ujiulize ni kitu gani umekifanya kwa wenzako",alisema Chikoka.


Umoja wa vijana wa CCM umeadhimisha Kitaifa miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara ambapo viongozi wa chama hicho Kitaifa wameshiriki wakiwemo wajumbe wa baraza kuu la UVCCM Taifa,Wenyeviti wa UVCCM mikoa mbalimbali.


Wenyeviti wa UVCCM waliofika Tarime katika maadhimisho hayo ni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika mkoa wa,Songwe,Mbeya,Dodoma,Geita,Tanga,Dar es salaam,Njombe,Tabora,Mara,Kilimanjaro,Pwani,Simiyu,Lindi,Shinyanga,Mwanza,Kigoma, Unguja kusini,Unguja kaskazini,na Unguja mjini magharibi.


Wajumbe wa baraza kuu UVCCM wameshiriki kutoka mkoa wa Kagera, Pemba kusini,Kigoma,Dodoma,Singida,Mwanza, Pemba kaskazini,Unguja mjini Magharibi,Njombe, Unguja kusini,Unguja kaskazini,Geita,Rukwa na Mbeya.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments