GGML WAMWAGA SH MILIONI 90 MKUTANO WA MADINI


KAMPUNI ya uchimbaji wa madini ya dhahabu mkoani Geita (GGML) imetoa msaada wa Sh milioni 90 kudhamini Mkutano wa nne wa Uwekezaji wa Madini na Madini mwaka huu unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini unafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia Februari 21 hadi 23 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo jijini Dar es salaam.

Aidha, msaada huo wa GGML ambao unaifanya kampuni hiyo kuwa mfadhili mkuu unajumuisha ukodishaji ukumbi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa muda wote wa mkutano huo pamoja na matangazo yanayohusu hafla hiyo.

Akizungumzia udhamini wa kampuni hiyo mwaka huu jana jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo ameishukuru serikali kuonesha dhamira ya wazi katika kuinua sekta ya madini.

Pia ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kuzingatia sheria na taratibu na kwa kuendelea kuwa moja ya inayoongoza kwa kulipa kodi na mapato mbalimbali ya Serikali.

“Sekta ya madini imenufaika kutokana na ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa miaka kadhaa. Katika kukuza maendeleo, GGML imejipanga kuendelea kushirikiana na serikali ili kuleta manufaa kwa pande zote mbili pamoja na wadau wengine,” alisema.

Aliongeza kuwa ana matumaini makubwa kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania.

“Malengo yetu yanaendana na yale ya serikali kwamba sekta ya madini inapaswa kuchangia angalau asilimia 10 kwenye pato la taifa (GDP) ifikapo mwaka 2025 na pia kuleta manufaa mapana kwa jamii,” alisema.

Katika hafla kama hiyo mwaka jana, GGML ilitambuliwa na serikali kama kampuni iliyofanya vizuri zaidi katika sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

GGML ilishinda tuzo hiyo baada ya kupata alama za juu zaidi katika kipengele cha uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira na usalama, kampuni inayongoza kwa kulipa kodi na mapato ya serikali na kampuni inayoongoza kwa kutoa biashara kampuni za ndani.

Hafla hiyo ya mwaka jana iliongozwa na Makamu wa Rais wa wakati huo (sasa Rais) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya GGML imeendelea kuwekeza nchini kwa zaidi ya miaka 20 na imefanikiwa kuwa kampuni ya mfano wa Sekta ya Madini nchini Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post