SERIKALI YATENGA BILIONI 1 KUENDELEZA WABUNIFU WA MAKISATU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiongea na Waandishi wa habari leo Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya wiki ya MAKISATU 2022.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiwa na wadau wa MAKISATU
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiongea na Waandishi wa habari Leo Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho ya wiki ya MAKISATU 2022

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA.

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza wabunifu watakaotambuliwa kwenye mashindano ya kitaifa ya Sayansi (MAKISATU)yanayotarajiwa kuanza tarehe 15-20 Mei,2022 Jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa leo Februari 16,2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu kuanza kwa maadhimisho ya wiki ya ubunifu na mashindano ya kitaifa ya MAKISATU 2022.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa wiki hiyo ya ubunifu inayoandaliwa kwa kushirikiana na programu ya UFUNGUO ya UNDP itafanyika katika mikoa 17 nchini ambayo ni Dar Es Salaam,Dodoma, Mbeya,Arusha,Mwanza,Iringa,Tanga, Kilimanjaro na Njombe.

Mikoa mingine ni Kigoma,Ruvuma,Mara,Mtwara,Kagera, Morogoro na Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine kitaifa  itaadhimishwa jijini Dodoma  sambamba na kilele cha MAKISATU.

"Wiki hii ni muhimu sana ambayo Serikali ya awamu ya sita inaichukulia kama sehemu ya mkakati wa kuongeza hamasa ya matumizi ya Sayansi , Teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii,"amesema.

Amefafanua kuwa katika kilele cha MAKISATU kutakuwa na maonesho ya Teknolojia na ubunifu,bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi zitakazoshiriki zikiwemo za kitafiti na maendeleo,vyuo vikuu,kumbi za ubunifu,Taasisi za kibiashara,Wakala wa Serikali, Wizara na taasisi binafsi yatakayoenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa wabunifu 21 watakaoshinda.

Prof. Mkenda pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kupitia MAKISATU 2019,2020 na 2021,Wizara imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,785 ambapo kati yao 466 walikidhi vigezo, kutambuliwa na kuhakikiwa.

"Bunifu mahiri 200 tayari zinaendelezwa na Serikali ili kufikia hatua ya kubiasharishwa,niwaeleze pia kuwa kati ya bunifu zinazoendelezwa na Serikali ,26 zimeshafikia hatua ya kubiasharishwa,wakati 95 ziko katika hatua ya sampuli kifani huku nyingine zikiwa Katika hatua za awali za kuandaa sampuli kifani,"amefafanua Waziri Mkenda. 

Waziri Mkenda pia ameeleza malengo ya wiki ya MAKISATU kuwa ni kuibua ,kutambua, kuendeleza jitihada zinazofanywa na wabunifu nchini na kuhamasisha matumizi ya Sayansi na Teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambapo kupitia maadhimisho hayo wabunifu watapata nafasi ya kutangaza bidhaa zao.

Kadhalika ameleeza kuwa licha ya kwamba usajili wa ubunifu kwa ajili ya mashindano hayo kufikia kikomo tarehe 10,Februari,2022,mahitaji bado ni makubwa hivyo kuongeza muda wa usajili wa wabunifu hadi tarehe 28, Februari,2022 .

"Hadi kufikia jana tumesajili wabunifu zaidi ya 480 kwa ajili ya mashindano,bado tunahitaji wabunifu wengi zaidi ,natoa wito kwa wabunifu nchini kuendelea kujisajili  kushiriki MAKISATU 2022,mwongozo wa fomu ya maombi zinapatokana kwenye tovuti za wizara yetu,"amesema.


 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post