MWANZA PRESS CLUB NA SHIRIKA LA INTERNEWS WAADHIMISHA SIKU YA REDIO JIJINI MWANZA

Na Mwandishi wetu - Mwanza

Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la Internews wameadhimisha siku ya Redio Duniani kwa kuwaleta waandishi wa habari pamoja na kujadili nguvu ya redio kwenye jamii za pembezoni.

Akifungua maadhimisho  hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel alisema kuwa, vyombo vya habari ikiwemo redio vina jukumu kubwa la kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zilizo na ukweli  na zinazowapa nafasi ya kujua uhalisia wa jambo ulivyo kupitia redio.

Aidha ameeleza umuhimu wa waandishi wa habari kufuata maadili yao ya kazi ili kuilinda jamii dhidi ya migogoro isiyo ya lazima.

Pia kulikuwa na uwasilishaji wa mada mbalimbali mbele ya waandishi wa habari zilizojikita kwenye kuonesha mchango wa redio kwenye kuleta maendeleo Nchini Tanzania.

Kwenye wasilisho lililoandaliwa na Edwin Soko na kuwasilishwa na Bi. Rose Mwanga lilionyesha kuwa, redio ina nguvu kubwa kwani inawaleta viongozi wa Serikali, AZAKI na wananchi pamoja na kuzungumzia mambo mbalimbali na utatuzi wake .

Pia wasilisho lilichambua umuhimu wa redio na teknolojia ulivyoongeza tika kwenye karne ya 21.

Naye Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano toka Internews Shaban Maganga alieleza umuhimu wa siku ya redio Duniani na mchango wake ulivyo mkubwa kwa jamii.

Siku ya redio Duniani uadhimishwa kila ifikapo Februari 13 ya kila Mwaka, na kwa kuwa siku hiyo itakuwa jumapili MPC na internews wameamua kufanya maadhimisho hayo leo Februari 11,2022.

Washiriki wa maadhimisho hayo walitoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo redio na kufanyika kwenye ukumbi wa Bismark Hotel ya Gold Crest.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments