AMUUA DADAAKE MADAI YA KUROGWA AKOSE NGUVU ZA KIUME

Picha haihusiani na habari hapa chini
**
Mwanafunzi wa Darasa la Saba Shule ya msingi Mwenge iliyopo Kata ya Kingolwira Manispaa ya Morogoro,Faidhat Ibrahimu (13) ameuawa kwa kukatwa mapanga na kaka yake.

Tukio hilo lilitokea Februari 15, 2022 usiku ambapo mtuhumiwa wa mauaji hayo anadaiwa kutoweka.

Akizungumzia tukio hilo leo mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Morogoro, Alpha Meela amesema chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa mirathi pamoja na imani za kishirikina.

"Kutokana na maelezo ya awali kwa watu ambao tumewahoji wanadai kuwa mtuhumiwa ana tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume na hivyo alikuwa akimtuhumu mama yake mdogo (mama wa marehemu) kuwa ndio amemroga," amesema Meela.

Ameongeza kuwa binti huyo alikatwa mapanga wakati akiwa jikoni anaandaa chakula cha usiku na alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro.

Amesema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo polisi walifika katika eneo la tukio ambapo mama mzazi wa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi lakini pia kwa usalama wake kutokana na jamii kukasirishishwa na tukio hilo.

Chanzo - SiteTv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments