WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA TUZO YA KISWAHILI KWA WASHINDI



**********************

Na. John Mapepele, WUSM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa leo Januari 27, 2022 ametoa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati -Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa washindi wa mwaka 2021 jijini Dar es Salaam.

Katika kundi la Riwaya Halfani Sudy ameibuka kuwa mshindi wa kwanza, Mohamed Omary ameibuka mshindi wa kwanza kundi la shairi, wakati Mbwana Kidato ameibuka mshindi wa pili katika kundi la tamthilia na Lukas Lubungo kuwa mshindi wa pili kwenye kundi la hadithi za kubuni.

Amesema dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ya kutekeleza mkakati wa kubidhaisha lugha ya Kiswahili Kitaifa na Kimataifa, ambao utazinduliwa hivi karibuni itafanikiwa ikiwa wadau wote watajitoa kwa dhati kutekeleza mkakati huu na kusimamia maendeleo ya lugha hii adhimu na aushi.

Mhe. Majaliwa amezipongeza kampuni za SAFAL na ALAF kwa kufadhili tukio hilo na ametoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano huo kwa kuwekeza katika lugha hiyo, huku akisisita kuwa kuwekeza katika Kiswahili itakuwa ni njia mojawapo ya kurudisha fadhila kwa wananchi ambao ndio wateja wa bidhaa hiyo.

Aidha, Mhe Majaliwa amesema Kiswahili kimetambuliwa kimataifa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kutangaza tarehe 7 mwezi Julai, kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani ambapo ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanza kuandaa wiki ya maadhimisho ya kiswahili katika siku ya mwaka huu.

Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake itashirikiana na wadau mbalimbali kukuza lugha ya kiswahili ili kufika sehemu mbalimbali duniani.

Mhe. Mchengerwa ameelekeza wadau mbalimbali wa lugha ya hiyo kuhakikisha wanaisherekea kwa namna ya pekee siku ya kiswahili ya Julai 7 mwaka huu kwa namna ya kipekee ili kuthibitishia dunia kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la lugha hiyo.

Katika halfa hiyo, Waziri Mkuu Mhe Majaliwa na Mhe. Mchengerwa walitumia nafasi hiyo kumtakia heri ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa wimbo wa kiswahili wa heri ya kuzaliwa uliongozwa na Jaji Mkuu wa tuzo hizo Profesa Aldin Mutembei kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post