UWT MWANZA : WANAOTOA MATAMSHI YA KUMKWAMISHA RAIS SAMIA WALAANIWE VIKALI


Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa Mwanza umetoa tamko kali la kulaani baadhi ya viongozi ambao wameanza kutoa matamshi yanayolenga kukwamisha jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Tamko hilo limetolewa Januari 05, 2022 na Mwenyekiti wa umoja huo, Hellen Bogoye wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa wale wote wanaotoa matamshi hayo wanapaswa kulaaniwa vikali.

“Wanaosema nchi itauzwa kisa kukopa wanapaswa kulaaniwa kwani mama (Rais Samia) anakopa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na tunaona miradi mbalimbali inavyotekelezwa ikiwemo madarasa ya viwango kote nchini”, ameonya Bogoye.
Katika hatua nyingine umoja huo kupitia kwa Mwenyekiti Bogoye umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba aliyoitoa Januari 04, 2021 Ikulu jijini Dar es salaam wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 ambapo pamoja na mambo mengine alisema nchi itaendelea kukopa kwa ajili ya maendeleo.


“Tunampongeza Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na anavyojali wananchi wake. Ana muda mchache madarakani takribani miezi minane lakini amefanya mambo mengi ya kuushangaza ulimwengu” amesema Bogoye wakati akipongeza hotuba ya Rais Samia.


Aidha Bogoye ameongeza kuwa Rais Samia hapaswi kukatishwa tamaa na maneno ya watu wanaotaka nchi hii isiendelee. “Naomba sana viongozi wenzetu mifumo dume iwatoke kwenye vichwa vywao, sasa hivi tunaangalia viongozi wenye uwezo, awe mwanamke ama mwanaume apewe madaraka. Mama (Rais Samia) anao uwezo, iweje watu wachache wamkashfu?” amehoji Bogohe na kuongeza;


“Kwa kweli wanawake wa Mkoa wa Mwanza tuko na mama (Rais Samia) bega kwa bega iwe mvua iwe jua na tutawapinga vikali wale wote wanaojaribu kumrudisha nyumba” amekemea Bogoye.
Kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia, Bogohe amesema shukurani pekee wanawake wa Mkoa Mwanza na nchi nzima wanayoweza kumpatia Rais Samia ni kumpigia kura kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Katika hatua nyingine, Bogoye amesema wale wote wanaotoa matamshi ya kejeli na kukimbilia kuomba msamaha wanapaswa kuacha mara moja akisema ili kukomesha tabia hiyo chama (CCM) kinapaswa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanaotoa matamshi hayo.
Tamko la UWT Mkoa Mwanza linakuja siku chache baada ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kunukuliwa akikosoa mpango wa Rais Samia kukopa fedha kwa ajili ya maendeleo akisema nchi ikiendelea kukopa ipo siku itauzwa ambapo hata hivyo alijitokeza na kuomba radhi akisema alinukuliwa vibaya na mitandao ya kijamii.
Tazama video hapa chini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments