POLISI WATUMIA MABOMU YA MACHOZI KUTAWANYA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA KARUME


Polisi mkoani Dar es Salaam wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyabiashara wa soko la Karume (Mchikichini) ambao wameandamana na kufunga barabara iliyopo karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla wakishinikiza kuruhusiwa kuendelea na biashara katika soko hilo lililoungua usiku wa kuamkia jana Jumapili.

Wafanyabiashara hao maarufu machinga wamefunga barabara hiyo muda mfupi baada ya kuandamana mpaka kwenye geti la kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam huku wakidai kuwa wanataka RC Makalla atoe tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.


Kabla ya kufunga barabara, wafanyabiashara hao ambao baadhi yao walikuwa wamebeba mabango waliandamana huku wakiwa wanaimba “Tunataka Soko letu” wakiwa wamezingira geti la ofisi hiyo, ikiwa ni siku moja imepita tangu soko hilo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija aliwaomba wafanyabishara hao kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliotangazwa na Serikali kwamba waiachie kamati ifanye kazi kwa siku saba na kutoa ripoti badala ya kuandamana kutaka kushindana na Serikali.


“Mnatakiwa kujiongeza pamoja na kwamba mnadai haki lakini lazima mfuate utaratibu Jana Waziri tuiachie Kamati ifanye kazi na walete ripoti tunaomba kuweni na subira,” aliwasihi.


Jana Jumapili baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla aliwataka wafanyabiasha wa soko hilo kuwa watulivu huku akiahidi kuundwa kamati ambayo itachunguza chanzo cha moto huo kwa siku 14 akipiga marufuku shughuli zozote kuendelea wakati wa uchunguzi huo.


Muda mfupi baada ya RC Makalla kutoa tamko hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa aliagiza kamati hiyo kufanya uchunguzi kwa siku saba badala ya 14.

Via>> Global Publishers

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments