MPAKA SASA MAKADA 9 WAMEJITOSA KUWANIA USPIKA WA BUNGE
Wanachama tisa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu za kuwania nafasi ya uspika wa Bunge kupitia chama hicho, kumrithi Job Ndugai aliyejiuzulu wiki iliyopita.


Akizungumza jana kwa niaba ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka, Katibu Msaidizi Mkuu Idara ya Oganaizesheni wa chama hicho, Solomon Itunda alisema wanachama hao waliochukua fomu hizo jana Dodoma ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Mbunge wa Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi, Dk Saimon Ngatunga, Tumsifu Mwasamale, Merkion Ndofi na Abwene Kajula.

Waliochukua fomu ofisi ndogo za CCM Dar es Salaam ni aliyewahi kuwa Waziri wa Madini, Stephen Masele, Hamidu Chamani na Patrick Nkandi.

Kwa ofisi ya Zanzibar hakuna mwanachama aliyechukua fomu hadi jana.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Dk Tulia alisema ni haki yake kikatiba kugombea nafasi ya uspika na kuomba wanachama wa CCM kumuunga mkono.

“Nimeshajaza fomu na kuirejesha, ni haki yangu kikatiba kugombea nafasi hiyo,” alisema.

Dk Tulia alisema ametumikia nafasi ya Unaibu Spika kwa muda wa miaka sita na amepata uzoefu wa kutosha.

Naye Kunambi alisema ameamua kugombea nafasi hiyo kwani uwezo anao na alishakitumikia chama na serikali.

Alisema aliwahi kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Siha, Mwanasheria wa CCM kwa muda wa miaka mitano na Mkurugenzi wa Jiji Dodoma kwa muda wa miaka minne.

“Naahidi kuwa Spika wa viwango kwani nina elimu ya shahada ya kwanza ya sheria na shahada yangu ya pili ni ya utawala wa umma, naamini wabunge wenzangu wa CCM wataniunga mkono,” alisema.

Uchukuaji fomu kupitia CCM ulianza jana na unatarajia kukamilika Januari 15, mwaka huu.

Baada ya uchukuaji na urejeshaji fomu kukamilika, Januari 17, mwaka huu Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa wagombea waliojitokeza kuomba kiti cha uspika.


Januari 18 hadi 19 kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu itafanya kazi hiyo.

Aidha, Januari 21 hadi 30, mwaka huu, kikao cha chama cha wabunge wa CCM kitapiga kura kumpata mgombea ambaye atakwenda kusimama bungeni kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge.

Ndugai alijiuzulu baada ya kutoa kauli ya kupinga serikali kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kusababisha mjadala mitandaoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post