MAELFU WAJITOKEZA KUAGA MIILI YA WAANDISHI WA HABARI WALIOFARIKI KWA AJALI YA GARI




NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza

MAELFU ya wananchi wa Jiji la Mwanza jana wamejitokeza kuiaga miili ya waandishi watano wa habari waliofariki kwa ajali ya gari juzi katika Wilay ya Busega, mkoani Simiyu.

Waombolezaji hao waliongozwa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.

Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 14 na majeruhi kadhaa,ilitokea majira ya saa 12:30 katika Kijiji cha Shimanilwe, Kata ya Kabita wilayani Busega, mkoani Simiyu ikihusisha gari namba SKT 8140 na gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T 281 DER mali ya Lunyenya Kaswalala.
Miili ya marehemu hao iliagwa jana kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza baada ya kuwasili uwanjani hapo majira ya saa 3:52 na kuibua vilio na simanzi kutoka kwa ndugu,jamaa na waombolezaji.


Waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni Ofisa Habari Mkoa wa Mwanza, Abel Ngapemba, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Steven Msengi, Johari Shani wa Uhuru Digital,Husna Mlanzi wa ITV, Anthony Chuwa wa Daily News Digital pamoja na dereva wa gari hilo Paul Silanga.

Pia waandishi wawili Tunu Herman na Ivvany Charles wa Icon TV walijeruhiwa na wamelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando wakiwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) ambapo wanaendelea vizuri.

Miili ya marehemu hao iliagwa jana kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza majira ya saa 6:30 hadi saa 8:25 na kuibua vilio na simanzi kutoka kwa ndugu,jamaa na waombolezaji ambapo mwili wa Husna Mlanzi ulizikwa katika makaburi ya Kirumba.

Marehemu wengine miili yao ilisafirishwa ambayo ni ya Abel Ngapemba na Steven Msengi (Dar es Salaam), Johari Shani (Arusha),Anthony Chuwa (Moshi) na Paul Silanga (Tabora) .

Akitoa salamu za pole kwa wafiwa na waombolezaji,Nape aliwaagiza waajiri wote waliokuwa wakidaiwa mishahara na marehemu hao wahakikishe wanawalipa stahiki zao ndani ya siku 7 kuanzia jana.

Alisema kuwa tutawakumbuka marehemu hao kwa kazi yao ya uzalendo; “Ni siku ngumu kidogo kwangu kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,ni shughuli yangu ya kwanza na ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari Kanda ya Ziwa,Mkoa wa Mwanza lakini kubwa pia kwa nchi yetu,”alisema Waziri huyo wa Habari.

Alisema kutokana na msiba huo mkubwa, amekuja kuwasindikiza mashujaa hao waliofia kazini wakitekeleza majukumu yao,pia wenzao wanafanya kazi hapa kwa huzuni nao wamekuja kuwasindikiza.

Nape alisema Sheria ya Wana Habari na Haki zao iliundwa wakati akiwa Waziri wa Habari wakati huo,lengo lilikuwa kuifanya tasnia hiyo kuwa taaluma inayoheshimika na haki zao.

Alisema kuwa amerudi nyumbani kusimamia sheria hiyo ya Huduma na Haki ya Habari na kuwahakikishia wana habari kuwa haki zao zitalindwa.

“Penye mapungufu yatarekebishwa ili kukidhi mahitaji na matakwa kwa kutengeneza mazingira ya kuwawezesha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru,viwango na weledi,” alisema Nape.

Waziri huyo wa habari alitumia fursa hiyo kuwaagiza waajiri wote waliokuwa wakidaiwa mishahara na marehemu hao kuanzia leo (jana) wahakikishe wanawalipa hata kama kama ni kukopa wakakope.

“Natoa siku 7 kwa waajiri wote wanaodaiwa na marehemu mishahara,kakope,kauze kama mwanahabari ambaye ni marehemu anakudai kakope ulimpe stahiki yake (familia zao zilipwe kuanzia leo), kutolipa haki za watu (waandishi wa habari) ni kuvunja sheria,umemwajiri mtu mlipe yawezekana wanapitia hali ngumu,”alisema.

Kuhusu matukio mengi ya ajali kwenye misafara ya viongozi kuwaandama na kuwagusa wanahabari Nape alisema viongozi wa juu wameliagiza jeshi la polisi kupeleka taarifa za ajali hizo.

Alieleza kuwa lengo la kuhitaji taarifa ya ajali hizo itawezesha kuchukua hatua y kuweka itifaki ya kuwalinda wana habari ingawa zipo sababu nyingi.

“Serikali inataka kujiridhisha ni kwa nini ajali hizo zinawagusa wana habari na haya nitayasimamia na kuhakikisha yanatekelezwa,”alisema Nape.

Alisema Wizara inatoa pole kwa waandishi wa Mwanza, na kwamba marehemu hao watakumbukwa kwa kazi zao na hasiti kuwaita mashujaa kutokana na kufia kwenye uwanja wa mapambano wakipigania taifa lao ambapo alionyesha kuguswa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa upendo aliounyesha kwa wana habari.

Aidha akitoa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan,Nape alisema kuwa ameguswa sana na msiba huo wa wana habari watano na anatoa pole kwa wafiwa,waombolezaji na wana habari wote.

Kwamba walikuwa vijana wadogo na wazazi wao waliwekeza kwao na baada ya kuanza uwekezaji huo maisha yao yamekoma ambapo pia Rais Samia aliwaombea majeruhi wa ajali hiyo wapone,wainuke na kurudi kwenye majukumu yao.

Kwa mujibu wa Nape viongozi waliotoa salamu za pole ni Mkamu wa Rais Dk. Philipo Mpango na Rais wa Zanzibar,Dk. Hussein Mwinyi,ambaye alimwomba Mwenyezi Mungu azipokee roho za marehemu hao na kuwaponya majeruhi, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wa wizara mbalimbali za serikali.

Awali Mkurugenzi wa UTPC Abubakar Karsan na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko,walisema uwanja wa kufanyia kazi si mzuri kutokana na sheria zinazosimia tasnia ya habari na kuomba kuhakikisha maslahi ya wanahabari yanalipwa na kuhskikishiwa usalama wao.

“Haki na usalama wa wana habari ni muhimu,wenzetu wamelala pale,baadhi hawajalipwa stahiki zao hata wanaofanyakazi hapa,hatulipwi sababu ya waajiri hawana moyo wa kutulipa kwa kisingizio kuwa biashara imeharibika wakati tunakutana nao kwenye baa hizo za bia zinatoka wapi,”alihoji Karsan.

Aliongeza kuwa; “Uwanja wa kufanyia kazi si mzuri sababu ya sheria kandamizi, Mkuu wa Mkoa (RC) Mhandisi Gabriel,amefanya huruma ya kutusaidia kwenye msiba huu na suala la usalama wa waandishi na maslahi yao hili liko kwako na yawezekana Mungu kakurudisha ukamilishe kazi hiyo,”alisema.

Mkurugenzi huyo wa UTPC alitumi fursa hiyo kumweleza Nape kuwa waajiri ambao marehemu baadhi wanawadai kabla hawajazikwa, yaleyale Mwenyezi Mungu awafumbue vichwa vyao wawalipe.

Soko yeye alisema marehemu hao ni majemedari wa vita waliofia kwenye uwanja wa vita huku akirejea katiba ya nchi kuhusu haki ya kupata na kutafuta habari na kumwomba Nape aangalie namna ya kulegeza baadhi ya vifungu vya sheria kuhusu viwango vya elimu kwa wana habari ikiwezekana wajiendeleze wakiwa kazini lakini pia kuboresha maslahi yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alisema hana nguvu ya kuzungumza kutokana na msiba huo mkubwa ulioligusa taifa na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya marehemu hao kwani maisha yana mwanzo na mwisho na kamwe wana habari hao hawatasahaulika.

Alisema heshima ya Mwanza na maendeleo yake yametokana na jeshi la waandishi wa habari mahiri,makini na wenye weledi wanaoipenda kazi yao na hilo amelishuhudia kwa miezi 6 baada ya kuhamia Mwanza.

“Bila waandishi wa habari kazi zetu ni sifuri (hazitambuliki),marehemu hawa waliipenda kazi yao,walibeba na kutembea na kalamu zao,walitumia sauti zao kuhoji na kuziweka vizuri, hawakulalamika wala kunung’unika licha ya shida walizo nazo,”alisema Mhandisi Gabriel.

Alisema liko tumaini kwa waliojiandaa kumcha Mungu, hivyo awaondolee adhabu awape nafasi waliomcha kwa kushika imani na ipo siku tutakuwa nao tukitambua zawadi ya uhai tuliyopewa na kuwaomba waombolezaji na wafiwa wasikate tama kwani Mungu ametupa matumaini ya kuubeba msiba huo.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema habari mbaya huletwa na wana habari na kila kazi ina mtego, hivyo ujio wa Waziri wa Habari kwenye msiba huo si bahati mbaya bali Mungu ana makusudi yake na kuwataka watumishi wa umma kutenda haki kwa watu wote.

“Watumishi wa umma tendeni haki, msidhulumu watu na heri kuiendea nyumba yenye msiba kuliko yenye sherehe, hivyo wote tumche Mungu tuitwe watakatifu.Htutawasau kamwe wana habari hao maisha yao yana mwanzo na mwisho ambapo jana (juzi) ilimpendeza Mungu ikawa mwisho wa maisha yao,”alisema.

Katika kuagwa kwa miili ya marehemu hao kulitanguliwa na dua la sala kutoka kwa Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Sheikhe Hassan Kabeke,Mchungaji Charles Mkumbo wa TAG na Padri George Nzuri wa Kanisa Katoliki kutokana na marehemu kuwa imani za madhehebu matatu tofauti.

Sheikhe Kabeke akitoa pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na waombolezaji pamoja na serikali, alisema marehemu hao walifanya kazi ya kuitumikia jamii kwa moyo wa unyenyekevu.

“Lakini pia Mhandisi Gabriel,naomba Mungu amtie nguvu n ujasiri kwa msiba huu, pia Rais Samia katika kipindi hiki kigumu na katika kuliongoza taifa na kuwatumikia Watanzania,”alisema.

Kwa upande wake Padri Nzungu alisema waandishi wa habari wakiwemo marehemu waliofariki kwa ajali wanafanya kazi ya uaminifu na utakatifu ya kuwatetea haki za watu na kupatanisha licha ya mitikisiko wanayoipata.

Alisema hata Mungu aliwatumia watu mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii, kazi ambayo pia inafanywa na wana habari nchini ya kuhakikisha jamii ifahamu mambo mengi yakiwemo ya maendeleo.

“Wana habari wanafanya kazi ya utakatifu,ni watu wa kupatanisha watu,wanaudhiwa kwa ajili ya haki, wanapata mitikisiko lakini Mungu anasema ufalme wa Mungu ni wao.”

“Injili ya Mathayo inasema heri wenye huzuni watafarijiwa, heri wenye njaa maana watashibishwa,wenye moyo safi watamwona Mungu na watakaoudhiwa kwa ajili ya haki ufalme wa mbinguni ni wao,” alisem Padri Nzungu.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Julius Peter,alisema walipokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko maubwa kutokana na kupoteza wanahabari hao wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi.

Alisema kazi ya Mungu haina makosa, ingawa tuliwapenda na tulitamani kuendelea kuwa nao lakini imempendeza Mungu kawapenda zaidi hivyo familia zao, ndugu,jamaa na marafiki waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments