MKURUGENZI TARIME ASEMA UANDIKISHAJI WA WATOTO HAUAMBATANI NA GHARAMA YOYOTENa Dinna Maningo, Tarime.

MKURUGENZI wa Halmashauri ya mji Tarime Bi Gimbana Ntavyo amesema kuwa uandikishaji wa watoto wenye umri wa kuandikishwa shule darasa la awali na darasa la kwanza hauambatani na gharama yoyote.

Ntavyo ameyasema hayo kupitia tangazo alilolitoa Januari 7,2022 baada ya baadhi ya wazazi kulalamika kutozwa michango wanapofika shuleni kuandikisha watoto wao.

Mkurugenzi huyo aliwatangazia Wazazi na Walezi wote wenye watoto wenye umri wa kuandikishwa shule kuwapeleka ili waandikishwe na kuanza masomo yao pindi shule zitakapofunguliwa tarehe 17,01/2022.

January,5/2022 Malunde 1 Blog iliripoti habari ikieleza wazazi kumlalamikia Nkongo Wandiba ambaye ni mkuu wa shule ya msingi Buguti kata ya Turwa wilayani humo kuwatoza fedha sh 5,000 pindi wanapofika shuleni kuandikisha watoto nakwamba kwa wale wazazi wasiokuwa na fedha hutishiwa watoto kutosajiliwa hadi pale watakapolipa fedha.

Ilielezwa kuwa mkuu huyo wa shule uomba sh.5,000 kati ya fedha hizo sh. 3,000 ni mchango wa ujenzi,1,000 pesa ya mlinzi na 1,000 pesa kwa ajili ya kuandaliwa kadi ya matokeo mwanafunzi anapofanya mtihani ambapo alieleza kuwa pesa hizo zilipitishwa na wazazi katika kikao cha Februari,2021 pamoja na ofisi ya wilaya.

Hata hivyo wazazi na Wenyeviti wa mitaa walipinga kuwa hakuna kikao kilichoketi kujadili na kupitisha michango na kwamba uamuzi huo umefanywa na mkuu wa shule nakuzuia wazazi kutolipa fedha kwakuwa hakuna vikao vilivyoketi na kutoa maamuzi wazazi kuchangia fedha.

Akisisitiza suala hilo,Mratibu Elimu kata ya Turwa Imani Buchafya alisema kuwa Desemba 6,2021 kiliketi kikao cha wakuu wote wa shule kwenye kata hiyo ambapo wakuu wa shule walitakiwa kutowachangisha wazazi michango wala kuwabughudhi watoto kuhusu michango nakuahidi kufatilia kwa kile alichoeleza kuwa hajapokea taarifa ya wazazi kuchangishwa fedha.


Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Turwa Marwa Timoro (Sheby) alikiri kupokea malalamiko ya wazazi kuombwa 5,000 wanapoandikisha watoto na akapiga marufuku michango kwa wanafunzi wanaoandikishwa nakwamba iwapo kuna uhitaji wa michango taratibu zifuatwe ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wazazi.

Januari,6,2022 aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa( TAMISEMI) ambaye kwa sasa amehamishiwa Wizara ya Afya Ummy Mwalimu akizungumza na vyombo vya habari alisema kuwa Maafisa wa wilaya na mkoa watawajibika kwa suala lolote itakapobainika shule zilizo kwenye wilaya zao na mikoa yao zinatoza ada na michango kwa ajili ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza.

Waziri Ummy aliongeza kuwa kama kuna michango itakayopaswa kuchangishwa ni lazima taratibu zifuatwe na kibari kitatolewa na mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments