SERIKALI KUWABAINI WATU 200,000 WANAOISHI NA VVU BILA KUJUA



MCHAKATO wa kuwapata watu 200,000 waishio na virusi vya Ukimwi bila kujua ni mbinu mojawapo ambayo Wizara ya Afya imesema itaitumia ili kupunguza maambukizi mapya na kufikia malengo ya milenia mwaka 2030.

Pamoja na hayo Wizara imesema inakusudia kupunguza idadi ya watoto wachanga wanaozaliwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka 6000 wanaozaliwa kila mwaka kwa kuhakikisha inamfikia kila mwanamke mwenye ujauzito.


Hayo yamesemwa jana Alhamisi Januari 20, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizindua mpango mkakati wa miaka mitano ya tafiti na mafunzo katika masuala ya afya ya jamii na lishe.

“Nchini Tanzania inakadiriwa watu milioni 1.7 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi lakini wanaotambua hali zao za afya ni milioni 1.5 pekee, hii ni changamoto kwetu lazima tuwatafute hawa 200,000 kwani ndiyo wanaochangia maambukizi mapya bila kujua.

“Tutawapata hawa kwa kuwashauri na kuhamasisha ili wapime kupitia mtaa kwa mtaa, kata kwa kata, halmashauri kwa halmashauri lazima tuhakikishe tunamaliza ugonjwa huu Tanzania ifikapo mwaka 2030. Mpaka sasa wanaotambua hali zao ni asilimia 88, wanaotumia dawa ni asilimia 98 na waliofanikiwa kufubaza makali ya virusi ni asilimia 92,” amesema Waziri Ummy.

Amesema suala la mtoto kuzaliwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi halikubaliki. “Matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona watoto wote wanazaliwa na afya njema pasipo virusi vya ukimwi, kaswende wala homa ya ini, hii ni changamoto kwetu lazima tuwatafute wote tuwapime na tukiwabaini tuwaingize kwenye dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” amesema.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Donald Wright amesema kati ya vipaumbele ambavyo ubalozi wa Marekani umewekeza ni kusaidia tafiti za masuala ya ukimwi kupitia Usaid na mafunzo pamoja na tafiti za masuala ya afya na lishe.

Chanzo - Global Publishers

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments