MHUDUMU WA GESTI AUAWA KWA KUKABWA SHINGO KWA KAMBA YA VIATU CHUMBANI KWA MTEJA
MHUDUMU wa nyumba ya kulala wageni ya Peace Lodge iliyoko katika eneo la Matarawe Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambaye jina lake limehifadhiwa anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 23 amekutwa amekufa kwenye moja ya vyumba vya kulala wageni.

Akizungumza na Nipashe jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Louis Taisamo, alisema tukio hilo limetokea juzi jioni ambako inadaiwa kuwa kwenye nyumba hiyo chumba namba nne mhudumu huyo, mkazi wa Kimoro-Makambi Manispaa ya Songea alikutwa akiwa ameuawa kwa kukabwa shingoni na kamba ya viatu na mtu asiyefahamika kwa jina, ambaye alikuwa ni mpangaji katika chumba hicho.


Alisema inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alipanga chumba namba nne kwa siku tano kuanzia Januari 6, mwaka huu hadi Januari 10 mwaka huu na baada ya hapo alitoweka na hakuwa analala katika chumba hicho.


Kamanda Taisamo alifafanua kuwa inadaiwa mtuhumiwa huyo alitoweka kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni baada ya kuwa na deni la pango Sh. 50,000 ambapo alilazimika kuacha simu yake aina ya Nokia na baadhi ya nguo zake mpaka hapo atakapolipa deni.

Alieleza zaidi kuwa inadaiwa mtuhumiwa huyo alikuwa akifika katika nyumba hiyo ya wageni mara kwa mara kuomba arudishiwe simu na nguo zake na alikuwa akijibiwa na mhudumu (marehemu) kuwa mali zake zipo kwa mmiliki wa nyumba hiyo na kwamba atarudishiwa mali zake baada ya kulipa deni.


Alisema inadaiwa siku ya tukio mtuhumiwa ambaye jina lake halijafahamika, alifika tena kwenye nyumba hiyo na kuwasiliana na mhudumu ambapo baada ya kutekeleza mauaji alitoroka na kufanikiwa kuondoka na vitu vyake ambavyo vilikuwa vimezuiliwa.

 Taisamo alisema mtuhumiwa hajakamatwa, na kwamba Jeshi la Polisi mkoani humo linafanya juhudi za kumtafuta.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post