ADAIWA KUMUUA MKE WAKE KWA KUMKATA KICHWA NAYE AJIUA JUU YA MTI


MICHAEL Methew mwenye umri wa miaka 33 mkazi wa Kijiji na Kata ya Mashete wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa anadaiwa kumuua mke wake kwa kumkata kichwa na kukitenganisha na kiwiliwili na kisha kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia mnyororo aliokuwa akitumia kufungia ng'ombe wake.

Tukio hilo limetokea Januari 4,2022 majira ya saa 12:30 jioni katika Kijiji cha Mashete ndani ya Kata ya Mashete wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mashete, Bosko Wazamani akizungumzia tukio hilo amesema kuwa,chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.

Wazamani amesema,mpitanjia mmoja alifika katika nyumba yao na ndipo alipokuta mwili wa mwanamke huyo ukiwa umelazwa sakafuni.

Amesema kuwa, wanandoa hao walikuwa wakiishi peke yao nje ya mji, na walikuwa wameoana miezi michache iliyopita hivyo hawakuwa na mtoto isipokuwa mwanamke alikuwa na mtoto aliyezaa na mwanaume mwingine, hata hivyo hakuwa akiishi na mtoto huyo.

Mtendaji huyo amesema, baada ya uongozi wa kijiji kufika katika nyumba hiyo walikuta mwili wa mwanamke huyo ambaye jina lake bado halijafahamika ukiwa umetengenishwa na kichwa na pembeni kukiwa na shoka likilotapakaa damu alilotumia mume wake kufanya mauaji hayo.

Viongozi hao wa serikali ya kijiji na kata, walipoanza jitihada za kumtafuta mtuhumiwa, walikuta mwili wake ukiwa unaning'inia kwenye mti jirani na nyumba yake, huku akiwa amejinyonga kwa kutumia mnyororo anaofungia mifugo yake.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, William Mwampaghale alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika kwa kuwa hakuna wa kumuhoji, lakini alisema kuwa polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

Amesema kuwa, inadhaniwa huenda mwanamke aliyeuawa alikuwa na mawasiliano na mzazi mwenzake kitendo kilichosababisha wivu wa kimapenzi kwa mume wake mpya na kuamua kufanya mauaji hayo.

Kamanda huyo amewaasa wakazi wa mkoa wa Rukwa kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi badala yake wawe wanawahusisha ndugu, wazee wa kimila na viongozi wa kidini kutafuta suluhu katika changamoto za ndoa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments