JWTZ YATOA ONYO WANAOPOTOSHA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII 'YOUTUBE


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za kupotosha ambazo zimekusudia kuwahadaa Watanzania kupitia mitandao ya Kijamii hususan YouTube, kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anaingilia kati sakata la Mhe. Rais na Spika. Jambo ambalo siyo la kweli.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linasikitika na linawaomba wananchi kuzipuuza taarifa zilizowekwa kwenye mtandao huo kupitia kwenye channel inayojiita NEWS 24 zenye kichwa cha habari ‘‘KIMENUKA MKUU WA MAJESHI MABEYO ATOA AMRI NZITO KUJIUZULU KWA NDUGAI’’ na ‘‘MKUU WA MAJESHI MABEYO AINGILIA KATI SAKATA LA RAIS NA SPIKA’’.

Ukweli ni kwamba, kikundi cha watu wachochezi kimetoa taarifa za uongo na uzushi kwa kutumia sauti isiyo ya Mkuu wa Majeshi huku wakiwaaminisha Umma kuwa ni sauti ya Jenerali Mabeyo kwamba aingilia kati sakata la Mhe. Spika.

JWTZ linawaomba Umma wa Watanzania kutoziamini taarifa hizo na wazipuuze kwa kuwa ni taarifa za uzushi na uchochezi zinazotungwa na kusambazwa na kikundi cha watu wasioitakia mema nchi yetu kwa maslahi yao binafsi.

Mkuu wa Majeshi hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na yaliyozushwa kwenye mitandao kwa kuwa JWTZ halijihusishi kwa njia yoyote ile na masuala ya kisiasa na kamwe halitafanya hivyo.

JWTZ linatoa onyo kwa wale wote wanaotumika kumchafua Mkuu wa Majeshi, kwa lengo la kutaka kuliingiza Jeshi kwenye siasa.

 Kamwe watu hao hawatafumbiwa macho na pindi watakapobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine.

Tunawaomba watanzania wote kuungana kwa kuendelea kupuuza na kukemea vikali taarifa hizo ambazo hazilitakii mema Taifa letu.


Nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kwamba JWTZ lipo imara, linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa Katiba kulinda na kuimarisha mipaka ya nchi yetu.

 Aidha, JWTZ linatekeleza majukumu yake ya msingi na lina mipaka yake kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Daima JWTZ litamlinda na kumtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu.

Limetolewa na:
Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

1/Post a Comment/Comments

Post a Comment