WAZIRI WA FEDHA : DENI LA TAIFA NI HIMILIFU...HAKUNA ATAKAYEGONGEWA MLANGO KUDAIWA


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa deni la taifa ni himilivu na kwamba hakuna Mtanzania yeyote atakayegongewa mlango wake ama kuamriwa kuuza mali yake ili kulipa deni la Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumanne, Januari 4, 2022 wakati akiwasilisha ripoti ya matumizi ya Fedha za Maendeleo (Fedha za Uviko-19) mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.


“Utekelezaji wa fedha imeendelea na kuongeza imani kwa Viongozi Wakuu wa IMF na kuamua kufuta masharti yote yaliyokuwa na riba kwa upande wa fedha zenye dirisha la ‘rapid financing instrument’ ambayo ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 378.17 sawa na theluthi mbili ya mkopo wote.


“Napenda kutumia fursa hii kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa mkopo wote wa Dola za Kimarekani 567.25 sawa na Trilioni 1.3 utakuwa mkopo usio na riba kabisa. Shirika la Fedha Duniani (IMF) limefuta masharti katika mkopo wa shilingi trilioni 1.3 na kwa maana hiyo, fedha tulizozichukua, baada ya kipindi cha mpito kupita tutazirudisha hizo hizo sh trilioni 1.3.


“Tathmini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba 2021 inaonesha deni letu ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu. Viashiria vinaonesha kuwa deni la serikali kwa uwiano wa pato la Taifa ni 31% ambapo ukomo wa kidunia ni 55%.


“Thamani ya sasa ya deni la nje kwa pato la Taifa ni 18.8%, ikilinganishwa na ukomo ambao ni 40%. Thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni 142%, ikilinganishwa na ukomo ambao ni 180%.


“Mhe. Rais wale wasiotambua kuwa unafungua uchumi ili watoto wao wapate ajira wataendelea kuyaelewa haya unayofanya siku ukifungua uchumi, biashara zikakua watoto wao wakapata ajira. Mkopo anapewa mwenye chanzo cha kulipa.


“Kwa hiyo mkopo ni biashara, tajiri na tajiri wanafanya biashara, biashara ya kutumia fedha hizo. Kwa maana hiyo, tutaendelea kukopa ili tutekeleze miradi mikubwa kwa uharaka. Mkopo wa serikali yako wa kwanza ni huu wa trilioni 1.3 ambao hauna riba, mikopo mengine ya serikali ni ile ya Banki ya Dunia ambayo imesainiwa siku nyingi na ulipaji wake ni hadi pale itakapoiva.


“Watu wengine wakisikia neno mkopo wanashtuka, Mkopo sio Msaada, Mkopo anapewa mwenye chanzo cha kulipa , Maskini ambaye hana cha kulipa hapewi Mkopo..Kwa hiyo mkopo ni biashara, tajiri na tajiri wanafanya biashara, biashara ya kutumia fedha hizo. Kwa maana hiyo, tutaendelea kukopa ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa uharaka.


“Hakuna siku Mtanzania mmoja mmoja atagongewa mlangoni kwake kwamba unadaiwa fedha hizi kwa sababu nchi yako ilikopa, hakuna. Pia, Marais hawakopi, ni serikali. Hili si jambo la familia, ni jambo la serikali,” amesema Mwigulu.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments