JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA, KUMPA MWANAFUNZI UJAUZITO


Na Amiri Kilagalila,Njombe
MAHAKAMA ya wilaya ya Njombe imemuhukumu Bright Peter Dismas (25) mkazi wa Kitisi halmashauri ya mji wa Makambako kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili likiwemo la ubakaji na kumpa ujauzito mwanafunzi.

Hukumu hiyo imetolewa jana na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Njombe Isack Mlowe ambapo amesema mshtakiwa huyo alimbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17 wa shule ya sekondari Mkilima iliyopo mjini Makambako.

Alisema tukio hilo la ubakaji lilitokea mwaka jana mwezi Februari katika mtaa wa Kitisi halmashauri ya mji Makambako.

Amesema mshtakiwa alianzisha mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi huyo ambapo siku ya tukio alikwenda nyumbani kwao akiwa peke yake.

Amesema baada ya kufika nyumbani hapo mshtakiwa huyo aliingia ndani na kuandaliwa chakula na mwanafunzi huyo kisha baadae wote wakaenda chumbani na kufanya mapenzi.

Amesema ilipofika mwezi oktoba mwaka jana mwanafunzi huyo aligundulika kuwa na ujauzito baada ya kufanyika vipimo shuleni kwa wanafunzi wote wa kike.

"Mwanafunzi huyo baada ya kugundulika kuwa na ujauzito alihojiwa ndipo akaeleza mahusiano yake na mshtakiwa" alisema Mlowe.

Amesema mshtakiwa huyo alihukumiwa kulipa fidia ya shilingi 1,000,000/= kama fidia kwa mwanafunzi huyo baada ya kutoka gerezani.

Wakili wa serikali Matiko Nyangero aliyekuwa akiendesha shauri hilo la jinai Namba 198/2020 aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na katika kutoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 130 (1) (2) (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2019, ambavyo mshtakiwa ameshtakiwa navyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments