SERIKALI YATOA BIL 11.92 KUWEZESHA KIUCHUMI WANAWAKE, VIJANA NA WENYE ULEMAVU DODOMA

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Fatma Mganga akiongea na wajasiriamali katika kikao cha tathmini ya Utekelezaji wa sera ya Uwekezaji wananchi kiuchumi jijini Dodoma.
Baadhi ya wajasiriamali waliohudhuria kikao cha tathmini ya Utekelezaji wa sera ya Uwekezaji wananchi kiuchumi kilichofanyia Katika ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa Dodoma.
Mke wa Waziri mkuu mstaafu Tunu Pinda(Kushoto)akifuatilia kwa umakini majadiliano katika mkutano wa uwezeshaji kiuchumi Dodoma.

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog, DODOMA.

SERIKALI imetoa mikopo yenye  thamani ya shilingi bilioni 11.92 kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanawake,vijana na wenye ulemavu wa Mkoa wa  Dodoma kwa kipindi cha Mwaka 2017/2018 hadi Novemba 2021.

Hayo yaeelezwa jana Jijini Dodoma na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Fatma Mganga wakati akiongea kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa sera ya uwekezaji wananchi kiuchumi kilichowashirikisha wanawake wajasiriamali,wenye ulemavu na wadau mbalimbali wa masuala ya maendeleo.

Akieleza katika kikao hicho ameeleza fedha hizo zilizotolewa katika Halmashauri za Bahi,Chamwinio,Chemba,Dodoma Jiji ,Kondoa ,Kondoa mji,Kongwa na Mpwampwa ambapo 7,004,724,612 zilielekezwa kwa wanawake,shilingi 4,264,231,059 kwa vijana na  Shilingi  652,795,298 kwa watu wenye ulemavu.

Ameeleza kuwa  kutokana na fedha hizo  jumla ya wanawake 12,427 wamenufaika huku wanaume 2,249 wakinufaika na kueleza kuwa wanawake wameonyesha kuwa na ufanisi mkubwa katika kurejesha mikopo kwa (43%)wakifuatiwa na wenye ulemavu (35%)na vijana (28%).

"Fedha hizi zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo kuanzisha Viwanda vidogo vya machinjio ya kuku,kukamua Mafuta ya alizeti,kusaga unga wa sembe,kutengeneza majiko banifu na mama lishe,na mingineyo,"ameeleza.

Pamoja na hayo amesema fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali kwa vikundi vya wanawake, watu wenye ulemavu na vijana zimesaidia upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa makundi ambayo hayawezi kukopesheka kupitia Taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanawake wanaojiunga na bima ya afya.

"Mikopo hii imeleta mafanikio makubwa katika uchumi wa wanawake,wanawake wengi Sasa Wana ajira binafsi na hali ya maisha yao imeboreshwa Kwa kuwa wanapata fedha za ziada kupitia biashara zao binafsi,"amesema.

Kwa upande wake Katibu tawala Msaidizi anayeshughulikia sekta za uchumi Aziza Mumba ameeleza kuwa licha ya juhudi na mafanikio yaliyopo bado kuna upungufu wa rasilimali watu wenye weledi katika kusimamia utoaji na urejeshaji wa mikopo .

Ameongeza kuwa,kuna upungufu wa rasilimali fedha na vitendea kazi kwa ajili ya uendeshaji wa mikopo inayotolewa pamoja na idadi kubwa ya maombi ya mikopo ikilinganishwa na uwezo wa halmashauri husika jambo linalopaswa kushughulikiwa.

Akieleza tathmini ya utekelezaji sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika Mkoa wa Dodoma, amesema kuwa ili kuondokana na kadhia hiyo kila Halmashauri zinapaswa kubuni vyanzo  vipya vya mapato ya ndani ili kuongeza kiasi cha utoaji mikopo Kwa vikundi vya ujasiriamali vinavyoomba mkopo.

"Nashauri kuwepo na mafunzo ya uongezaji thamani ya mazao na kuunganishwa na mnyororo wa masoko kwa wanavikundi,ili kufanikisha hili lazima kuwepo na ubunifu wa mfumo wa Tehama ambao utasaidia kukumbusha waliokopa kurejesha fedha kwa muda na hatimaye kuwezesha wengine kukopa,"amesema.

Naye mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Tunu Pinda ametumia nafasi hiyo kueleza nafasi ya mwanamke katika uwekezaji kiuchumi ambapo alisema kutokana na wanawake wengi kuelimika na kukubali kujiingiza kufanya biashara hali zao za maisha zimeimarika.

Amesema,usawa wa kijinsia unaoendelezwa na Serikali umesaidia kwa kiasi kikubwa wanawake kujitambua na kukubali kuwezeshana wao kwa wao na kuondokana na dhana ya udhaifu iliyokuwa imezoeleka.

"Wanawake wengi wanaishi kwenye nyumba nzuri,wanasomesha watoto,wanazingatia usalama wa chakula na yote haya yanakuja kutokana na faida ya uwekezaji,kwa ujumla tuko mbele sana kiuchumi Kwa Sasa asilimia 50 ya wanawake wanamiliki akaunti za benki,"ameeleza mama Pinda.

Mbali na hayo amewashauri wanawake kuendesha biashara zao kwa kutumia mikopo kutoka Taasisi za mikopo yenye riba nafuu hali itakayo wakwamua kiuchumi.

Amesema yeye binafsi amekiwa akikopa kwenye Taasisi mbalimbali na kutumia fedha hizo kwenye masuala ya kilimo biashara na kusaidia kutoa ajira kwa wanawake wengine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments