RAIS SAMIA AONGOZA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo.
**
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amewaongoza Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania bara katika sherehe zilizofana zilizofanyika kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia aliwasili katika uwanja wa Uhuru akiwa kwenye gari la wazi pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo na kulakiwa kwa shangwe na maelfu ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo pamoja na wageni waalikwa.

Mara baada ya kuingia uwanja wa Uhuru Rais Samia alipigiwa wimbo wa taifa pamoja na kupigiwa mizinga 21 ya heshima na kisha kukagua gwaride la heshima la maadhimisho ya miaka 60 Uhuru lililoandaliwa na vikosi vya majeshi ya Tanzania na kisha kwenda kukaa katika jukwaa kuu.

Sherehe hizo za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania zilihudhuriwa na marais wastaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, wake wa waasisi wa taifa la Tanzania Mama Maria Nyerere pamoja na Mama Fatuma Karume.

Baadhi ya marais wa nchi jirani pamoja na wawakilishi wa wakuu wa nchi zingine walihudhuria sherehe hizo akiwamo mgeni rasmi wa maadhimisho hayo miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Azali Assoumani wa visiwa vya Comoro pamoja na Paul Kagame wa Rwanda.

Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post