WAHUNI 12 WANAOKWAPUA SIMU KWA BODABODA WAKAMATWAJeshi la Polisi katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya, imefanikiwa kukamata simu zaidi ya 30 na watuhumiwa 12 wa matukio ya uporaji wa simu, wengi wakiwa ni wale wanaotumia bodaboda na visu kufanya uhalifu huo.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika oparesheni maalum iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini Kenya katika maeneo ya Githogoro, Murera na Kiambu ambapo watuhumiwa hao, hujifanya ni madereva bodaboda kabla ya kuwapora abiria na watembea kwa miguu simu zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kiambu, Mohamed Badel amesema watuhumiwa hao, hufurika katika mitaa ya Mji wa Kiambu kuanzia majira ya saa kumi alfajiri hadi saa kumi na moja, muda ambao watu wengi hutoka majumbani mwao kuelekea makazini.

Badel amesema waliamua kuendesha oparesheni maalum baada ya kusikia malalamiko ya mara kwa mara ya wakazi wa mji huo ambapo kwa kushirikiana na wasamaria wema, walifanikiwa kuwanasa wahalifu hao.

Ameongeza kuwa watuhumiwa wote wapo rumande na wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Kiambu kusomewa mashtaka yanayowakabili na kuwataka madereva wa bodaboda wanaozingatia sheria, kujiandikisha na kupewa namba maalum zitakazowatofautisha na wahalifu.

Pia amewataka watu walioibiwa simu zao, kufika katika Kituo cha Polisi cha Kiambu ili kuzitambua simu zao.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments