WAZIRI MHAGAMA : BADO KUNA MAENEO YANAHITAJI NGUVU ZAIDI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,uratibu,Bunge,Kazi,Vijana ,Ajira na wenye ulemavu,Jenista Mhagama 

Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog Dodoma

LICHA ya kuwepo mafanikio katika mapambano dhidi ya UKIMWI Serikali imesema  bado kuna maeneo ambayo yanahitajika nguvu zaidi ili kudhibiti virusi vya ukimwi na Ukimwi na hatimaye kutokomeza Vvu na Ukimwi ifikapo Mwaka 2030 kama inavyoelekezwa katika malengo ya Kidunia.

Hayo yameelezwa leo  Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,uratibu,Bunge,Kazi,Vijana ,Ajira na wenye ulemavu,Jenista Mhagama wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayotatajiwa kufanyika kitaifa  Disemba Mosi Mwaka huu Mkoani Mbeya.

Waziri Mhagama ameyataja baadhi ya  maeneo ambayo yanatakiwa kuwekewa mkazo zaidi kuwa ni pamoja na kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi VVU  hasa kwa Vijana kwani zaidi ya theluthi  moja ya Maambukizi mapya hutokea kwa Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hususani Vijana wa kike.

Amesema ikiwa Vijana wataelekezwa namna ya kujikinga na maambukizi mapya na kukubali kujikinga,hali ya usambazaji virusi hivyo itapungua na itakuwa nafuu kwa Vijana wengine.

"Nawasisitiza vijana ukimwi bado upo,lazima kila mmoja akubali kumkinga mwingine hii itatusaidia kuokoa nguvu kazi ya taifa na kuipa unafuu Serikali katika kugharamia masuala ya ukimwi,"amesema.

Mhagama amefafanua kuwa Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU na Ukimwi ambapo kiwango Cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 ya makisio ya Watu wanaoishi na  Virusi vya Ukimwi (WAVIU)Mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 83 Mwaka 2019.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la  Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Nchini,Reticia Morris ameishukuru Serikali kwa kuwajali Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi hasa kwa kuwaletea chanjo ya Uviko19 ambayo ni muhimu kwao.

Maandalizi ya maadhimisho hayo yamekamilika na yataambatana na maonyesho ya shughuli za Wadau wa kudhibiti VVU na Ukimwi ambayo yataanza rasmi  Novemba 24 hadi Disemba Mosi Mwaka huu katika kiwanja Cha Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.

Aidha   Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na yanaenda sambamba na Kauli mbiu isemayo "zingatia usawa, Tokomeza Ukimwi,Tokomeza magonjwa ya mlipuko.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments