NAIBU WAZIRI MARY MASANJA : IDADI YA WATALII IMEANZA KUONGEZEKA TANZANIA


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog , Dodoma.

SEKTA ya utalii na Maliasili imesema kutokana na jitihada zake katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 idadi ya watalii imeanza kuongeza kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 Hadi kufikia 716,169 mwezi Oktoba mwaka huu.


Aidha imeliwezesha taifa kupata mafanikio kutokana na idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka katika Nchi mbalimbali duniani kuongezeka kutoka 9,847 mwaka 1960 hadi kufikia watalii 1,527,230 mwaka 2019.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amesema hayo jana Jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru na kuongeza kuwa kazi ya kuitangaza Tanzania isibaki kwa Serikali pekee bali kwa watanzania wote.


Amesema kumekuwepo na na ongezeko la mapato yatokanayo na watalii kwa ambapo kwa mwaka 1995 mapato yalikuwa Dola za kimarekani Milioni 259,44 ambapo yaliendelea kuongezeka hadi kufikia Dola za marekani bilioni 2.6 mwaka 2019 kabla ya ugonjwa wa UVIKO 19.

Amesema sekta hiyo ina umuhimu mkubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla katika Nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania na kwamba kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato ni moja ya mafanikio ya kujivunia kutokana na juhudi za Serikali za kuendeleza na kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii nchini.

Kadhalika amewataka Watanzania kutoa mchango kwenye sekta ya utalii nchini kwa kutangaza vivutio vyake katika mitandao ya kijamii,wawapo safarini na wanapokutana na wageni hali itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na maeneo ya hifadhi za wanyamapori,misitu na nyuki,malikale yenye mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira,ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi.


Amefafaua kuwa mchanganuo huo unatokana na uhifadhi wa mifumo ikolojia unaokidhi matakwa ya kimazingira,kijamii na kiutamaduni,kitaifa,kikanda na kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments