MILIONI 96 KUTUMIKA KUTOA ELIMU YA UHIFADHI KWA WANA VIJIJI BURIGI - CHATO

Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 96,725,600 kwa ajili ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi katika vijiji 38 vinavyoizunguka Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato vikiwemo vijiji 10 vya Wilaya ya Biharamulo ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kati ya wananchi na hifadhi hiyo baada ya kuingiza mifugo hifadhini. 

Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhe. Eng. Ezra Chiwesela aliyetaka kujua lini Serikali itatoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji hivyo. 

Mhe. Masanja amesisitiza kuwa Serikali imekuwa ikitoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaoishi jirani na Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato akitolea mfano katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilitumia shilingi milioni 20,836,200 kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji 37 vinavyoizunguka hifadhi hiyo na katika Wilaya ya Biharamulo vijiji sita vya Kiruruma, Nyabugombe, Ngararambe, Kabukome, Katerela na Kitwechembogo. 

Aidha, sambamba na hilo, Mhe. Masanja amesema Serikali itatumia makundi maalum ili kusaidia kusambaza elimu ya uhifadhi kwa jamii hiyo akitolea mfano viongozi wa dini, wanasiasa na wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari. 

Mhe. Masanja amewaomba Waheshimiwa Wabunge kuiunga mkono Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi. 

Kuhusu hoja ya Mhe. Chiwesela ya wafugaji kurudishiwa mifugo pungufu baada ya kukamatwa hifadhini na kulipishwa faini ya shilingi laki moja kwa kila ngo’mbe, Mhe. Masanja ameahidi kuwa Serikali itawachukulia hatua watumishi watakaogundulika kudhulumu mifugo ya wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments