MAHAKAMA YATUPA PINGAMIZI KESI YA FREEMAN MBOWE NA WENZAKE


Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imekubali kupokea barua inayomthibitisha Askari Mpelelezi, Ricardo Msemwa, kuwa ndiye aliyepokea kitabu cha mahabusu, kutoka kwa msajili wa mahakama hiyo.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, tarehe 15 Novemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joakhim Tiganga, akitoa uamuzi madogo wa pingamizi la mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake.

Mawakili wa utetezi, walipinga kielelezo hicho Ijumaa iliyopita, wakidai, shahidi aliyeomba barua hiyo ipokelewe hana uwezo wa kufanya hivyo kisheria, kwa madai nyaraka hiyo ililengwa mahususi kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), jijini Dodoma, na kuwa Msemwa siyo mtumishi wa ofisi hiyo hivyo barua hiyo haimhusu.

Pia, walidai shahidi huyo wa pili wa Jamhuri katika ushahidi wake, hakusema barua hiyo imemfikiaje na au kueleza uwepo wa jina lake katika nyaraka hiyo.

Jaji Tiganga amesema, mahakama hiyo imeipokea barua hiyo kwa kuwa ni nyaraka muhimu.

Jaji huyo amesema, mawakili wa utetezi watapima kuaminika kwa shahidi na au nyaraka hiyo wakati wa maswali ya dodoso.

“Kupokea nyaraka ni jambo moja lakini kupima uzito wa nyaraka ni jambo lingine. Katika kupima uzito wa nyaraka hiyo ni mahakama inaona kwamba ni wakati wa cross-examination.

“Kwa maana hiyo mahakama inaona barua hiyo iliyokuwa inaenda ofisi ya taifa ya mashtaka na kwamba shahidi alipewa nakala. Basi Mahakama hii inaona ni nyaraka sahihi na kwa sababu hiyo mahakama inapokea barua.

 “Upande wa utetezi wanayo nafasi wakati wa dodoso, wanaweza kumpima shahidi huyu kama mkweli au siyo mkweli. Kielelezo kinatakiwa kisomwe lakini ku- refer content- ili aweze kutambua nyaraka hiyo. Kwa hiyo basi kwa Kesi ya Robison Mwangisi siyo sahihi kutumika kwenye kesi hii.”

Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo imelitupa mbali pingamizi kwa kuwa sheria ya ushahidi inaruhusu shahidi kuaminika kupitia ushahidi wake alioutoa kwa mdomo, na kwamba mahakama hiyo imethibitisha kuwa Msemwa ni shahidi wa kuaminika.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments