GGML YAMWAGA MILIONI 248 KUWEZESHA WATUMISHI WAKE KUHITIMU SHAHADA YA UZAMILI



Watumishi wa GGML waliohitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Chuo hicho kwenye mafahali yaliyofanyika juzi jijini Arusha.
Ofisa mafunzo kitengo cha huduma na usalama kutoka GGML, Timoth Kihombo (kushoto) akipokea zawadi ya uongozi bora kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI), Profesa Bonard Mwape. Kihombo ni mmoja wa watumishi tisa wa GGML waliohitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka chuoni hapo kwa ufadhili wa kampuni hiyo.
Kutoka kushoto ni Mhandisi James Nzuamkende, Afisa Rasilimali watu, Hamza Ngunangwa na Meneja wa Fedha, Prudence Kami wakiwa ni kati ya watumishi tisa wa kampuni ya GGML waliohitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI), kwa ufadhili wa kampuni hiyo.
Ofisa wa Idara ya Fedha kutoka GGML, Gama Zephania Sogoni, ambaye ni mmoja wa wahitimu wa kike pekee waliohitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI), kwa ufadhili wa kampuni hiyo.
**


Na Mwandishi wetu

JUMLA ya watumishi waandamizi 18 wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) wamehitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Uongozi cha Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 248.

Hayo yameelezwa juzi na Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo wakati akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya ESAMI jijini Arusha ambapo watumishi tisa waandamizi wa Kampuni hiyo walihitimu.

Watumishi hao tisa wanafanya idadi ya watumishi waliofadhiliwa na kampuni hiyo ya GGML kuwa 18 tangu mpango huo wa masomo ulipoanza mwaka 2018.

Alisema hatua hiyo imeiwezesha GGML kuwa na watumishi kadhaa wa Kitanzania walioteuliwa kushika nyadhifa za juu.

Alisema hatua hiyo inaenda sawa na malengo ya kuifanya kampuni kuwa na watumishi wa Kitanzania wanaosimamia idara mbalimbali ndani ya kampuni na kutekeleza majukumu yako kwa uweledi na ufanisi mzuri.

“Kampuni imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kubaini vipaji vya watumishi wake watanzania hususani kupitia mpango stashahada ya uzamili (Postgraduate diploma) kutoka Shule ya Biashara ya Regenesys ya Afrika Kusini.

“Zaidi ya wafanyakazi 50 wa ngazi ya juu na wa kati wamefadhiliwa na kuhitimu programu hiyo tangu 2016,” alisema.

Alisema katika jitihada za kuwawezesha wanawake nao kushika nyadhifa za juu, GGML imebuni programu zinazowawezesha wanawake kupiga hatua.

“Kwa muda wa miaka minne iliyopita, idadi ya wafanyakazi wetu wanawake wameshiriki katika Mpango wa ‘Mwanamke Baadaye’ unaotekelezwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambapo wanne walioshiriki katika mpango huu wamehitimu mwaka huu.

“Kampuni pia inashiriki katika program ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi ambao unashirikisha vijana wa kike na wa kiume,” alisema.

Aidha, mmoja wa wahitimu tisa katika mahafali hayo, Mhandisi Mkuu kutoka GGML, Seif Maftah ambaye alihitimu Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara alisema ufadhili huo wa GGML umekuja wakati muafaka.

“Nimefurahi na ninahisi kuwa na bahati ya kipekee kupata fursa hii. Kampuni yetu imekuwa mstari wa mbele kuwaongezea uwezo watumishi wake mbali na faida na ushindani kwa rasilimali zake za ndani. Kozi hii imeniwezesha kuongeza ujuzi wangu, hasa usimamizi wa fedha,” alisema Mhandisi Maftah.

Naye Ofisa Rasilimali watu kutoka GGML, Hamza Ngunangwa ambaye pia amehitimu alisema, “Nimefurahi kuhitimu licha ya changamoto za COVID-19, nawapongeza ESAMI kwa kuanzisha madarasa ya mtandaoni. Hii ilitusaidia sana.

“Pia uongozi wa GGML ulitupatia likizo ya masomo ambayo ilituwezesha kukamilisha kozi hii. Lakini pia niwapongeze wahitimu wenzangu kwa kutiana moyo katika kipindi chote cha masomo yetu,” alisema.

Kwa upande wake Ofisa wa Idara ya Fedha kutoka GGML, Gama Zephania Sogoni, ambaye ni mmoja wa wahitimu wa kike pekee mwaka huu alisema furaha ya kuhitimu inahitimisha safari ngumu yenye manufaa aliyopitia.

“Ilinibidi nifanye kazi za ziada kupanga ratiba yangu kwa sababu mbali na kazi, nilikuwa natakiwa kusoma na kulea ujauzito wangu lakini sasa ninajivunia mafanikio haya. Haikuwa rahisi,” alisema Gama.

GGML imebaki kuwa kampuni inayoongoza kwa ulipaji kodi bora katika tasnia ya uziduaji nchini baada ya kulipa zaidi ya Sh trilioni 3.9 kwa Serikali tangu kuanzishwa kwake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments