NBS YAANZA MAANDALIZI YA MPANGO WA PILI WA KUBORESHA NA KUIMARISHA TAKWIMU NCHINI

Mtakwimu mkuu wa Serikaki Dkt.Albina Chuwa akiongea kuhusu maandalizi ya mpango wa pili wa kuboresha na kuimarisha Takwimu nchini

Na Dotto Kwilasa -Malunde 1 blog Dodoma

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanza maandalizi ya mpango wa pili wa kuboresha na kuimarisha Takwimu nchini (Tanzania Statistics Masterplan-TSMP II)unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2026/26.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wakati akiongea na Waandishi habari kuhusu maandalizi ya mpango huo na kueleza kuwa kwa sasa upo katika ngazi ya kitaalamu na kwamba ukikamilika utafuata taratibu zilizopo ndani ya Serikali kwa ajili ya kuridhiwa na kuanza utekelezaji wake kwa manufaa ya nchi.

Dkt. Chuwa amefafanua kuwa mradi huo utakaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 60 kwa nchi nzima kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara utajikita katika kulinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango wa kwanza ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zilizobakia.

Ameongeza kuwa mpango huo utajikita pia kuimarisha ukusanyaji na matumizi ya Takwimu za kiutawala zinazozalishwa zaidi a Wizara, Taasisi na Idara za Serikali kwa lengo la kuipunguzia gharama Serikali katika kufanya tafiti za kila baada ya miaka mitatu na badala yake tafiti hizo zitafanyika kila baada ya miaka mitano na kwa sensa kwa kila miaka 10.

"Chini ya Mpango huu wa pili,Wizara na Taasisi husika zitajengewa uwezo zaidi wa kitaalamu wa ukusanyaji na uchambuzi wa Takwimu,kupatiwa vifaa na ujenzi wa mifumo na kuunganisha Mfumo mama wa Taifa wa Takwimu, vile vile ukusanyaji na matumizi ya Takwimu za kiutawala zinazozalishwa kila mara na kupunguza idadi ya maswali Katika madodoso ya sensa,"amefafanua Mtakwimu huyo Mkuu wa Serikali.

Mbali na hayo amesema, mpango huo utajielekeza katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa takwimu katika Wizara,Idara na Halmashauri kwa ujumla na kuwezesha mfumo wa taifa wa takwimu kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya matumizi ya TEHAMA katika uzalishaji na usambazaji wa takwimu.

"Nitumie fursa hii kuwaomba wadau wote wa takwimu nchini ikijumuisha wazalishaji na watumiaji,kutoa mapendekezo yao kupitia vikao mbalimbali vilivyopangwa kufanyika ili tuweze kupata mpango bora wa kuboresha takwimu,"amesema.

Dkt.Chuwa ametumia nafasi hiyo kuiomba Benki hiyo ya Dunia kuona haja ya kutoa kipaumbele katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika mpango huo wa pili wa kuboresha takwimu nchini na kuiomba msaada wa angalai Dola za marekani milioni 80 ambazo zitatumika kwenye vifaa vya sensa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki hiyo Rob Swinkels amesema wao kama wadau wa takwimu wanatambua umuhimu wa Takwimu za kisasa na hivyo wanatumia nafasi hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mifumo ya takwimu na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazozalishwa takwimu bora Afrika.

"Tunatambua kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya takwimu kwa ajili ya kupanga Maendeleo,hivyo tutajikita katika maeneo ambayo yanahusika na kuyapa kipaumbele na hatimaye kufanikisha mpango huu unaotarajiwa kupima mwelekeo na hali za maisha ya watu,"amesisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments