JAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA DKT PAUL KIHWELO AFUNGUA MAFUNZO KWA WAWEZESHAJI WA MAFUNZO YA HAKI ZA WATOTO


Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto  katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.
Bi. Victoria Mgonela Mwakilishi wa UNICEF akitoa salamu kutoka Shirika la UNICEF nchini Tanzania kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma
Picha ya pamoja ya majaji wanaoshiriki katika mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto. Mafunzo haya yanafanyika katika ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma.
Picha ya pamoja ya majaji wanaoshiriki katika mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto na washiriki wengine waliohudhuria katika mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma
 Baadhi ya Washiriki wa mafunzo kwa wawezeshaji wa mafunzo ya haki za watoto wakiwa wanasikiliza mada zinazoendelea katika mafunzo hayo kutoka kwa muwezeshaji Mhe. Sophia Wambura Jaji Mstaafu (hayupo pichani)
****

Mhe. Dkt Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama leo amefungua rasmi mafunzo kwa wawezeshaji 36 wa mafunzo ya haki za watoto kutoka sehemu mbalimbali Tanzania. 

 Mafunzo haya yanafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 15 Novemba mpaka 19 Novemba katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma. 

Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya ufadhili wa Shirika linalohudumia watoto duniani (UNICEF).

Washiriki wa mafunzo haya ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu, Mahakimu wakazi wa ngazi mbalimbali, Waendesha Mashtaka na Maafisa Ustawi wa Jamii.

 Washiriki hawa watapitishwa katika mada mbalimbali zitakazowawezesha kuwa na uelewa na ujuzi wa pamoja juu ya uendeshaji bora wa mashauri ya mtoto.

Katika mafunzo hayo kutakuwa na mada mbalimbali zitawasilishwa na wawezeshaji mahiri na wabobezi katika masuala ya namna bora ya uendeshaji wamashauri hayo ambao ni Mhe. Sophia Wambura Jaji Mstaafu na Mhe. Matilda Philip Wakili Mstaafu wa kujitegemea.

Akiongea katika ufunguzi wa mafunzo haya Mhe. Dkt. Kihwelo alielezea lengo kubwa la mafunzo haya kuwa ni kuwajengea uwezo wadau wanaoendesha mashauri ya mtoto. 

Kundi hilo linalofundishwa mafunzo hayo pia ni kwa ajili ya kuwaandaa ili waweze kufundisha wengine kwenye masuala ya haki za mtoto anapokuwa mhanga. 

Hii imekuja kwa ajili ya kuongeza kundi la wawezeshaji baada ya wengi waliofanya mafunzo ya namna hii kustaafu.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka UNICEF, Bi. Victoria MKgonela ameushukuru uongozi wa mahakama na Chuo kwa kulipa uzito wa kipekee suala la uendeshaji wa mashauri ya mtoto na kuahidi kuwa UNICEF itaendelea na mashirikiano hayo.

Mafunzo kama hayo yamewahi kuendeshwa mwaka 2014 ambapo ilijumuisha majaji 6, Mahakimu wakazi 6, maafisa ustawi wa jamii 2 na watumishi 3 kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments