WATANZANIA MILIONI 10 KUINULIWA KIUCHUMI KUPITIA TASAF

 

Na Dotto Kwilasa - Dodoma

SERIKALI imedhamiria kuinua hali za  kiuchumi za watanzania wote masikini kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kwa kizifikia  kaya zaidi ya 1,450,000/= ambazo kwa makadirio ya chini ni sawa na wastani wa watanzania 10,000,000/=.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa wakati akiongea na wanachi kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika ziara yake aliyoifanya hivi karibuni katika mikoa ya Kanda ya ziwa.

Amesema katika ziara hiyo changamoto nyingi zinazohusu TASAF ziliibuliwa ambapo baadhi ya walengwa walilalamika kutotambuliwa na kuingizwa kwenye mpango huo kipindi cha kwanza na cha pili cha awamu ya tatu na kucheleweshewa malipo kutokana na kutozingatia kalenda ya malipo, kuwepo kwa changamoto ya mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao pamoja na  kuingizwa kwenye mpango kaya ambazo hazina sifa.

Kufuatia hali hiyo,Waziri huyo amewaelekeza watendaji wa TASAF kupitia halmashauri za Wilaya zote nchini  kufuatilia malalamiko ya kaya ambazo hazikutambuliwa na kufanya uhakiki wa kaya zote ambazo hazikupata nafasi ya kutambuliwa na kuandikishwa katika mazoezi ya utambuzi yaliyokamilika hivi karibuni katika vijiji,mitaa na shehia zote.

Aidha,ameagiza malipo kwa kaya masikini yafuate kalenda ya malipo na kutochelewa ili kutumia vizuri ruzuku zao katika mahitaji ya msingi na kufanya shughuli za kukuza uchumi wa kaya ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kina kubaini changamoto zote na kuzipatia suluhisho na hatimaye walengwa walipwe kwa njia ya taslimu na kwa wakati.

Wakati huo huo amezungumzia kwa upande wa Utumishi wa Umma na kusema kuwa  changamoto zilizobainika ni pamoja na watumishi wengi kutozingatia sheria,kanuni na taratibu za kiutumishi huku akitoa wito kwa watumishi hao kuzingatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa jumapili tarehe 10,Oktoba 2021 kuhusu mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

"Nitoe wito kwa watumishi wa Umma ambao ndiyo watekelezaji wakuu wa mpango huu kutekeleza kwa uadilifu,weledi,uzalendo na kwa juhudi kubwa ili kufanikisha kwamba mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na mafanikio makubwa,muda wa utekelezaji wa mpango huu ni miezi tisa tu,"amesisitiza. 

Aidha ameeleza kuwa utendaji kazi wa watumishi watakaotekeleza miradi hiyo utapimwa kwa jinsi watakavyotekeleza miradi kwa uaminifu,uadilifu,weledi na kwa wakati na kwamba wao kama wizara yenye dhamana ya utumishi na utawala bora watahakikisha kwamba maelekezo hayo ya Rais yanatekelezwa kikamilifu.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amesema katika kukabiliana na upungufu wa Wahandisi nchini,Ofisi yake imetoa kibali cha ajira 260 kwa ajili ya kujaza nafasi wazi katika Mamlaka za Serikali za mitaa.

Amesema,kwa upande wa watendaji wa kata,mtaa na vijiji tathmini ya mahitaji halisi imeshafanyika na michakato ya kuandaa ajira hizo unaendelea.

Pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuwaelekeza waajiri kuendelea kushughulikia watumishi wenye vigezo na sifa za kupandishwa cheo Kwa kiwatengea bajeti katika mwaka wa fedha ujao na kujiridhisha kuwa watumishi wote wanaostahili kutengewa bajeti ya kupandishwa vyeo wanatengewa nafasi.

"Waajiri wote nchini,wanapaswa kushughulikia madai ya watumishi na malimbikizo ya mishahara,hakikisheni mnaingiza madai ya malimbikizo ya mishahara katika mfumo wa HCMIS Kama ilivyoelekezwa katika waraka wa Utumishi wa Umma,"amesema.

Pia amewataka waajiri wote kuwasilisha orodha  za watumishi Wenye sifa za kukaimu ili Ofisi hiyo iweze kukamilisha mchakato wa kujaza nafasi wazi za idara na vitengo.

"Hapa napenda kusisitiza kuwaajiri waepuke kufanya upendeleo na unyanyasaji kwa watumishi kwa kuwakandamiza na kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao kwa amani,"amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments