SHIRIKA LA MEDO LAWEZESHA SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI, SINGIDA


Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakionesha mabango yenye jumbe mbalimbali katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika Wilaya ya Singida

Na Edina Malekela,Singida.
WAZAZI/Walezi wametakiwa kuwatafutia njia mbadala watoto wao wa kike ya kujikwamua kiuchumi inapotokea kukatishwa ndoto zao kwa kushindwa kuendelea na masomo kwasababu mbalimbali ikiwemo kubebeshwa mimba.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili alitoa wito huo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika kiwilaya katika mji mdogo wa Ilongero wilayani Singida.

Muragili alisema siku hiyo inapaswa kuchukuliwa kwa umuhimu wake kwani inaenda kuleta mapinduzi makubwa ya kumkomboa mtoto wa kike kutokana na wazazi kupata uelewa juu ya haki za mtoto.

"Jamii zetu huko nyuma hazikuwa zinawapa fursa mtoto wa kike hasa haki ya kupata Elimu,lakini baada ya kuanzishwa siku hii kwa mara ya kwanza mwaka 2012 imesaidia kwa kiasi kikubwa na tumeona mtoto wa kike akishika nafasi mbalimbali za kiuongozi", alisema Muragili.

Aliwaambia mapambano ya kumkomboa mtoto wa kike hayawezi kufanikiwa kama wazazi hawatashiriki kikamilifu katika mapambano hayo kwa kuwafichua wanautekeleza vitendo vya ukatili,hivyo amewaomba wazazi kushiriki kikamilifu.

"Halafu Wazazi tujitahidi sana kuwatimizia watoto wetu hasa watoto wa kike mahitaji yao ili wajiepushe kuingia kwenye tamaa zitakazo wapelekea kushindwa kufikia malengo yao", alisema Muragili.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Esta Chaula aliwataka Wazazi kujitahidi kugawa majukumu sawa yatakayompa nafasi mtoto wa kike ya kupata mahitaji mengine kama fursa ya Elimu kwani licha ya Serikali kutoa Elimu bure bado kumekuwa na changamoto ya Wazazi kukandamizwa kwa kupewa majukumu mengi ya kufanya huko kwenye familia.

"Wazazi tuwe karibu na watoto wetu na hii itatusaidia kuona mapema mabadiliko ya watoto wetu na kuyadhibiti mapema kabla yayajaleta madhara." alisema Chaula.

Shirika la Maendeleo ya Elimu Mtinko (MEDO) lililopo mkoani hapa ndiyo limewezesha shughuli ya maadhimisho hayo yakienda sambamba na kauli mbiu yake "Kizazi cha kidijitali, Kizazi chetu"

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi muhamasishaji kutoka Shirika hilo Emineema Peter alisema maadhimisho hayo yanalenga kuzitambua haki za mtoto wa kike na changamoto anazozipitia katika jamii ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Alisema wakati wa janga la COVID-19 limeharakisha majukwaa ya kidijitali ya kujifunzia,kupata na kuunganisha watu.watu bilioni 2.2 chini ya umri wa miaka 25 bado hawana huduma ya mtandao nyumbani,na wasichana wanauwezo mkubwa wa kukosa huduma hiyo.

Aidha alisema pengo la kijinsia kwa watumiaji wa mtandao ulimwenguni lilikua kutoka 11% mwaka 2013 hadi 17% mwaka 2019,katika nchi zilizoendelea zaidi duniani huzunguka karibu 43%.

Wanafunzi wakiwa kwenye maandamano wakionesha mabango yenye jumbe mbalimbali katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika Wilaya ya Singida

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments