KAMPUNI YA JADD YAZALISHA MBEGU BORA ZA KAHAWA NA KUZIGAWA BURE KWA WAKULIMA

 

Meneja wa Kampuni ya JJAD Kagera Farmer's Tanzania limited Aron Michael akitoa maelezo kwa mwananchi aliyefika katika Banda lake kujua kampuni hiyo inavyofanya kazi
**

Na Ashura Jumapili, Bukoba
Kampuni ya JADD Kagera Farmer's Tanzania limited,imeamua kuzalisha mbegu Bora za kahawa na kuzigawa bure kwa wakulima ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mbegu Bora zenye tija.

Hayo yamesemwa leo na Meneja wa kampuni ya JJAD Kagera Farmer's Tanzania limited Aron Michael wakati wa maadhimisho ya siku ya Kahawa mkoa wa Kagera.

Michael alisema kuwa kampuni yao imekuwa ikitoa mafunzo kwa Wataalamu wa kilimo walioajiriwa na serikali ambao pia wanakwenda kutoa elimu hiyo kwa wakulima.

Alisema baada ya wakulima hao kupata elimu ya kilimo chenye tija wanaandaa mashamba ambayo yanakaguliwa na wataalamu na kisha kutoa vibali kwa wakulima kwenda kwenye kampuni hiyo kuchukua Miche Bora ya Kahawa bure bila malipo.

Alisema Kahawa ni zao kubwa la kibiashara Mkoani Kagera hivyo kampuni imelenga kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaendelea kuongezeka kwa kuhimiza wakulima kupanda miche bora na yenye tija.

Alisema miche hiyo bora itasaidia kuongeza uzalishaji ambao utasaidia mkulima mmoja mmoja kuongeza kipato na taifa kwa ujumla.

Alisema sababu zilizokuwa zinapelekea uzalishaji mdogo ni pamoja na wananchi kuwa na mibuni ya asili ambayo ina umri wa zaidi ya miaka ( 40 )wakati uzalishaji mkubwa unakomea miaka ( 20- 25 ).

Alisema sasa wameleta miche bora ambayo itaanza kuzalisha kahawa kuanzia mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu na ikifikisha miaka kumi inaondolewa na kundwa Miche mingine.

Alisema kampuni hiyo kwa kutambua umuhimu wa uzalishaji wa kutumia miche bora yenye tija imekuwa ikiwapa fursa wakulima kujifunza mbinu za uzalishaji wenye tija zaidi.

Alisema msimu wa 2020/21 kampuni ilizalisha miche  1,574,000 na msimu wa 2021/22  walizalisha Miche  milioni 2 na kusambaza kwa wakulima mkoani humo.

Kwa upande wake Meneja wa bodi ya Kahawa mkoa wa Kagera Melkiad Masawe, alisema Oktoba mosi kila mwaka Duniani kote wadau wa Kahawa hukutana kujadili mambo mbalimbali ya mnyororo wa thamani kwa zao la kahawa.

Masawe, alisema lengo kuu ni hamasa matumizi endelevu na usawa wa kibiashara kwa zao la kahawa kutanua wigo na soko .

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Wezesha ushiriki wa Vijana na Wanawake kwa sekta endelevu ya Kahawa" alisema mwaka huu maadhimisho hayo yamepata mwamko mkubwa.

Alisema mkoa wa Kagera unaongoza kwa uzalishaji wa Kahawa safi kwa wastani wa Tani elfu  ( 25  Hadi 40 ) sawa na asilimia 50 ya Kahawa yote inayozalishwa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments