ATUPWA JELA MIAKA 15 KWA KUIBA NG'OMBE KAHAMA



Picha ya ng'ombe

Na Ali Lityawi, Kahama

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga imemuhukumu kifungo cha miaka 15 jela, Makoye Juma (19) mkazi wa Kijiji Cha Kangeme,Kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama, baaada ya kukutwa na kosa la wizi wa mifugo.

Akitoa hukumu,Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Christine Chovenye alisema mahakama inamtia hatiani mtuhumiwa Makoye kwa kuikutwa na kosa hilo la wizi wa mifugo kinyume cha kifungu namba 257(1) na kifungu namba (268)na (3) cha kanuni ya adhabu sura ya 16i.

Hakimu Chovenye alisema baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi kutoka upande wa mashitaka unamtia hatiani mtuhumiwa Makoye Juma na kutoa adhabu hiyo ya kwenda jela miaka 15 huku mshitakiwa namba mbili ambaye ni Shija Kagoma (29) akiachiwa huru baada ya ushahidi kutojitosheleza kumtia hatiani.

Alisema ushahidi upande wa Mashtaka hauna shaka tofauti na uliotolewa na upande wa utetezi ambao umejawa na dosari nyingi hivyo mahakama kujiridhisha mshitakiwa huyo aliiba mifugo aina ya Ngómbe wa watu wenye thamani ya shilingi milioni 1.9 mali ya Helena Msabila mkazi wa Kata ya Ushetu katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani hapa.

Aliendelea kusema baada ya Mahakama yake kupata ushahidi wa kutosheleza kutoka katika upande wa mashitaka inaamua kutoa adhabu hiyo kwa mtuhumiwa huyo ili kuwa fundisho kwa wananchi wenye tabia za wizi kama hizo.

Kabla ya hukumu hiyo Mwendesha mashitaka katika kesi hiyo, Mercy Ngowi, aliiambia mahakama hana kumbukumbu ya Mshtakiwa kama amepata kufanya makosa hapo awali,hata hivyo aliomba mahakama kutoa adhabu kali kwani matukio kama hayo yamekuwa yakifanyika mara kwa Mara katika jamii.

Kwa upande wake mtuhumiwa huyo aliiomba mahakakama kumpunguzia adhabu hiyo kwani ni mtoto pekee katika familia na kuongeza kuwa anaishi pamoja na bibi yake na wadogo zake ambao wamekuwa wakimtegemea katika maisha ya kila siku.

Katika hatua nyingine Mahakama hiyo pia imemuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Ester Makoye mkazi wa Masumbwe katika Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita kwa kosa la wizi wa kuaminiwa kinyume cha sheria namba 257(1) cha kanuni ya adhabu namba 273(b) sura ya 16.

Mtuhumiwa huyo aliaminiwa magunia 196 ya mpunga kutunza na Joyce Ibrahimu lakini akaamua kukoboa maguni yote na kuyauza kabla ya kutumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi.

Hakimu MKazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Christine Chovenye, alisema mtuhumiwa huyo aliaminiwa kutunza magunia hayo yenye thamani ya shilingi milioni 10 na Joyce Ibrahimu kabla ya kuyakoboa magunia hayo na kuyauza,kitendo ambacho ni kosa.

Chovenye alisema mbali na kifungo hicho cha mwaka mmoja jela kwa Mshitakiwa huyo, atalazimika pia kulipa kiasi hicho cha fedha pindi atakapomaliza kutumikia adhabu yake hiyo.

Mwendesha mashitaka katika kesi hiyo Mercy Ngowi aliiamba Mahakama kuwa alipomuhoji mthumiwa huyo alikiri kupokea kiasi hicho cha magunia ya Mpunga.



Katika kujitetea mahakamani hapo mtuhumiwa huyo aliiomba mahakama ya Wilaya kumpa adhabu ndogo kwa kuwa ana watoto wadogo ambao wanamtegemea hivyo mahakama hiyo imuonee huruma kwa kitendo alichokuwa amefanya.

Aidha mahakama hiyo katika kesi hiyo ilimuachia huru, Shija Kagoma (29) Mkazi pia wa Kangeme, baada ya ushahidi kutojitosheleza kumtia hatiani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments