MGEJA AMPONGEZA RAIS SAMIA KUINGILIA KATI BEI YA MABATI NA SARUJI KUPANDA

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja

Na Baltazar Mashaka - Kahama
MWENYEKITI wa Taasisi ya Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuingilia kati suala la upandaji holela wa vifaa vya ujenzi nchini.

Alisema Rais Samia anastahili pongezi baada ya hivi karibuni kugusia suala la kupanda holela kwa bei ya saruji,mabati na nondo, bidhaa zinazogusa maisha ya wananchi na hivyo kusababisha kuchangia kupanda kwa gharama za maisha hasa kwa wananchi wanyonge.

Alitoa pongenzi hizo jana ofisini kwake mjini Kahama, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mustakabali wa nchi pamoja na mambo mengine.

“Hatua alizochukua Rais Samia za kuingilia kati upandaji holela wa bei ya mabati,saruji na nondo na kumwagiza waziri mwenye dhamana kukaa na wenye viwanda (wazalishaji) kuangalia tatizo hilo na kulitafutia ufumbuzi,ni muhimu na ni jambo jema linalopaswa kupongezwa na Watanzania na kumwuunga mkono Mh.Rais,”alisema Mgeja.

Alisema kwa kitendo hicho ameonyesha dhamira yake njema kuona wananchi wake anaowaongoza wanamudu gharama za maisha na kuwa na maisha bora ya kuwawezesha kujiletea maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

“Pamoja na nia njema ya serikali kuruhusu soko huria na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kibiashara ili kulinda wawekezaji wa ndani,baadhi ya wafanyabiashara wanatumia fursa na kivuli cha uwekezaji kuwakandamiza wananchi kwa kuwapandishia bei ya bidhaa ovyo ovyo kila mara kwa visingizio mbalimbali,wanawasababisha washindwe kumudu gharama za maisha,”alisema Mgeja.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa Mkoa wa Shinyanga na Mjumbe wa NEC ya CCM Taifa,alisema tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wachache wanaotoaka kupata utajiri wa haraka wanalenga kuigombanisha serikali na wananchi ili waichukie serikali yao kwa sababu maisha ni siasa pia.

Mgeja alikwenda mbali zaidi kuwa licha ya vifaa vya ujenzi kupanda bei,eneo jingine lenye balaa kubwa ni la madawa ya binadamu ambapo yanauzwa kwa bei kubwa isiyoshikika kwa wananchi wa kawaida.

“Wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa za binadamu hawana huruma,dawa mbalimbali bei zake ziko juu sana na zinapanda bila kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya wananchi,”alidai Mgeja.

Aidha aliiomba serikali kumulika kwenye eneo hilo la dawa linalogusa pia maisha ya watu na uhai wa binadamu ili kuwapunguzia makali ya maisha.

Pia kupitia dawati la ushauri la Mzalendo Foundation, Mgeja aliishauri serikali kuwa ipo haja ya kuunda upya Tume ya Bei ili kufuatilia na kufanya ulinganifu wa bei za bidhaa kutoka viwandani ndani na nje hadi kuwafikia walaji ili kudhibiti ongezeko na upandaji holela wa bei kwenye bidhaa unapotokea.

“Kuna malalamiko mengi ya chini kwa chini kutoka kwa wananchi kuhusu bei za bidhaa kupanda holela, uwiano wa mapato na matumizi una tofauti kubwa,sasa soko huria lisipodhibitiwa linakuwa soko holela,lazima tuseme ukweli ili kuwanusuru wananchi,”alisema Mgeja na kuongeza;

“Ni vyema serikali ikalazimika kutoa bei elekezi kwenye bidhaa baadhi zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja yakiwemo madawa ya binadamu,haiwezekani kuuzwa bila wauzaji kudhibitiwa na TMD (Mamlaka ya Vifaa Tiba na Dawa) kama ilivyo EWURA inavyopanga bei elekezi ya nishati ya mafuta.”

Mgeja alisistiza kuwa wafanyabiashara hawana huruma na wananchi wanyonge wala masikini,hivyo kuwaacha wafanye biashara wanavyotaka,wanawaumiza walaji na ni imani yake kuwa maoni hayo serikali ya awamu ya sita itayafanyia kazi kwa vile ni sikivu,hivyo wananchi waendelee kuiunga mkono inapokabiliana na changamoto zinazogusa maisha yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments