MAHAKAMA YAWATOZA FAINI WAFANYABIASHARA WATANO KAHAMA KWA KUKIUKA TARATIBU ZA UTOAJI RISITI



Na Ali Lityawi - Kahama
Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama imewahukumu kutoa faini wafanyabiashara watano kwa nyakati tofauti kwa kutotoa risiti za mauzo pamoja na kuwazuia maafisa wa Mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa kikodi wa Kahama kutekeleza majukumu yao.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mahakama hiyo Christine Chovenye washtakiwa wawili Juma Saguda (40) mwenye kesi namba 254/2021 mkazi wa Nyasubi Manispaa ya Kahama pamoja Emanuely Kidenya (32) mwenye kesi namba 264/ 2021 , iliwatia hatiani baada ya kuridhika na maeleezo ya upande wa mashitaka.

Hakimu Chovenye akitoa hukumu kwa mtuhumiwa Saguda aliyehukumiwa kutoa faini ya shilingi 3,000,000/= ama kifungo cha kwenda jela miaka miwili,alisema mahakama imeridhika pasina shaka na maelezo ya upande wa Mashtaka,hivyo kutoa adhabu hiyo.


Naye Mshtakiwa Kidenya alihukumiwa faini ya kiasi cha shilingi Laki Moja na Nusu (150,000/- ) ama kwenda jela miaka miwili,baada ya mahakama kumtia hatiani kwa kosa la kuwazuia maafisa wa TRA kufanya kazi yao.

Wakiwakilishwa na Wakili wao Martin Masanja,waliiomba mahakama iwapatie hukumu hafifu baada ya wateja wake kukiri makosa yao na kwamba ilikuwa ni mara yao ya kwanza kutenda makosa hayo.

Wakati huo huo Mahakama hiyo pia imemuhukumu Salvatory Mihambo (35) mkazi wa Manispaa ya Kahama kulipa faini kiasi cha milioni tatu ama kwenda jela miaka mitatu,kwa kosa la kushindwa kutoa risiti baada ya malipo.

Katika kesi namba 250/2021 iliyofunguliwa mahakamani hapo mshtakiwa huyo alitiwa hatiani kwa kosa hilo baada kukubali kutoa ushirikino na kufanya kuipunguzia mahakama mrundikano wa mashauri na hivyo Hakimu Mkazi mfawidhi ya Mahakama ya Wilaya ya Kahama Fredrick Lukuna kutoa adhabu hiyo.

Wakili upande wa utetezi Godluck Herman aliiomba Mahakama kwa mteja wake kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na kuwa Kampuni yake bado ni changa katika Biashara aliyokuwa akifanya.

Katika kesi namba 260/2021,Hakimu Donasian Augustino alimtoza faini ya Shilingi Milioni Tatu ama kifungo cha kwenda jela miaka mitatu,Mshtakiwa Gervas Kamuhabwa(47)Mkazi wa Kahama kwa Kushindwa kutoa risiti baada ya kutoa huduma.

Mshtakiwa Kamuhabwa alikiri kosa na kuomba huruma ya mahakama kwa kuwa lilikuwa kosa lake la kwanza na kwamba yeye ni mlipaji mzuri wa Kodi za Serikali isipokuwa changamoto ya mtandao ndiyo iliyosababisha kutokea makosa hayo.


Aidha katika kesi namba 253/2021,Hakimu Mkazi huyo Donasian,alimhukumu kulipa faini ya Shilingi Milioni Tatu ama kwenda jela miaka mitatu,Mshtakiwa Benard Lyaka( 41 ) Mkazi wa Kahama Mjini,kwa kosa la kutotoa risiti baada ya malipo.

Akiwakilishwa na Wakili Martin Masanja,aliomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa kosa lake la kwanza,pia ana watoto pamoja na ndugu wanaomtegemea.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Donasian,alisema mahakama inamtia hatiani Mshtakiwa licha ombi la huruma alilotoa Mshtakiwa, hivyo inatoa hukumu hiyo ili liwe funzo kwa Mshtakiwa huyo na jamii kwa ujumla.

Katika kesi hizo zinazowakabili wafanyabiashara hao katika mahakama hiyo, wote walifanikiwa kulipa faini walizokuwa wametozwa na Mahakama na hivyo kuachiwa huru.

Hivi karibuni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa kikodi wa Kahama iliwafikisha mahakamani wafanyabiashara 12 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale ya kutotoa Risiti kwa wateja pamoja na kutotumia mashine za kielekroniki (Efds).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments