MFANYABIASHARA KAHAMA AHUKUMIWA JELA MIAKA MITATU KUTOTUMIA MASHINE YA EFD

Na Mwandishi wa Malunde 1 Blog - Kahama

Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Kahama,imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela Mfanyabiashara,Lucas Kishimbe,baada ya kukutwa na hatia ya kutoa huduma pasipo kutumia mashine ya kutolea risiti ya Kielekroniki (EFD).

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi,Donasian Augustino,baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Mashtaka.

Hakimu Augustino alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote ameridhika pasipo shaka yoyote kuwa Mshtakiwa kupitia Kampuni yake ya Kitapela Investment Limited amekuwa akitoa huduma za kibiashara bila kutumia mashine ya EFD.

Alisema anamhukumu faini ya Shilingi Milioni Tatu ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela ili kuwa fundisho kwa wafanyabiashara wengine wenye tabia hiyo wanaosababisha Serikali kutopata Kodi stahiki. 

Mfanayabiashara huyo alilipa faini hiyo.

Hata hivyo Wakili wa utetezi wa Mfanyabiashara huyo,Wakili Martin Masanja kutoka Kampuni ya Mawakili ya Lake Zone Attorneys,alisema mteja wake alikiri kutotumia vizuri EFD hivyo kumshauri kulipa faini.

Aidha katika Mahakama hiyo hiyo Hakimu Mkazi,David Msalilwa,alimhukumu faini ya Shilingi Milioni Moja na Nusu ama kwenda jela mwezi mmoja baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutoweka sehemu ya wazi mashine ya EFD.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akitetewa na Wakili Martin Masanja,alikiri kosa,hivyo kulipa faini ili kuepuka kifungo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kikodi Kahama,imewafikisha mahakamani wafanyabiashara 12 wa Wilayani Kahama,wakikabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kutonunua mashine za EFD,kutotoa risiti stahiki kulingana na gharama za bidhaa wanazouza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments