WAZIRI UMMY MWALIMU AFUNGA WIKI YA ASASI ZA KIRAIA 2021...ATAKA WAENDELEE KUTOA HUDUMA BORA


Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Mwalimu leo Alhamisi Oktoba 28,2021 akifunga Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Jijini Dodoma.

Na: Hughes Dugilo, DODOMA.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Mwalimu leo Alhamisi Oktoba 28,2021 amefunga Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Jijini Dodoma.

Katika hotuba yake mbele ya Wadau wa Serikali na Mashirika ya Asasi za Kiraia nchini ameahidi kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo na kuyasihi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni moja ya mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi.

“Kwa kutambua mchango wa Azaki natoa wito kwenu kuendelea kushirikiana na Serikali kuendelea kuihudumia jamii ambayo Asasi hizi mmekuwa mkifanya kazi nizuri kwa kuifikia jamii hasa wananchi walioko vijijini kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji na halmashauri" ,amesema Mhe. Ummy

Aidha ametoa wito kwa Sekta Binafsi kuwekeza kwenye mashirika ya Asasi za Kiraia ili kuchangia ukuaji wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla na kwamba kwa kufanya hivyo kutaisaidia Sekta Binafsi kutimiza malengo yao ya huduma za jamii kwani asasi hizo zimekuwa zikifanyakazi na jamii hizo kwenye maeneo yao.

Pia amezitaka Asasi za Kiraia kuongeza nguvu katika suala zima la kutoa elimu kwa wananchi na kuwajengea uwezo ili wananchi hao waweze kujisimamia katika shughuli zao za kimaendeleo na kiuchumi huku akiwataka kuwasaidia madiwani kwenye halmashauri kwa kuwajengea uwezo kwenye masuala mbalimbali yakiwemo usimamizi wa fedha na miradi ya maendeleo.

“Napenda kuwapongeza sana kwa elimu mnayotoa kwa wananchi kwa kuwajengea uwezo, lakini naomba muende mbali zaidi kuyafikia mabaraza ya madiwani kwenye halmauri zetu ili nao wajengewe uwezo wa kusimamia halmashauri kwenye matumizi ya fedha na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo”,ameongeza Mhe. Ummy.

Awali akitoa Salamu na kuelezea shughuli mbalimbali zilizofanywa na Asasi ya Kiraia kwenye Wiki ya Azaki, mratibu wa Wiki ya Azaki na Mshauri wa Foundation for Civil Society (FCS) Justice Rutenge ameeleza kazi zilizofanywa katika wiki ya Azaki ikiwa ni pamoja na mijadala mbalimbali iliyowakutanisha wadau wa Asasi za Kiraia, Wabunge, Makundi Maaalum na wananchi ambapo kwa pamoja waliweza kushirikiana katika mazungumzo na mijadala iliyolenga kujadili masuala yanayohusu ustawi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“Mheshimiwa Waziri Wiki ya Azaki mwaka huu imeweza kuzikutanisha Asasi zaidiya 300 ambao kwapamoja waliweza kukutana hapa Dodoma kuanzia siku ya ufunguzi na baadae kushiriki kwenye mijadala mbalimbali iliyowawezesha kutoa mawazo yao juu ya masuala mbalimbali ya ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla" Amesema Justice.


Wiki ya AZAKI ni jukwaa pekee nchini lililowaleta kwa pamoja wadau wakuu wa maendeleo ikiwemo Serikali, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia, pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa nchi na maendeleo ya Taifa ambapo yalizinduliwa rasmi leo Octoba 23 na Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb), na kufungwa rasmi leo Octoba 28, 2021

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments