UVCCM KAHAMA WAPONGEZWA KWA KUHAMASISHA MICHEZO

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Wadau wa michezo wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameupongeza uongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa kuhamasisha watu kufanya mazoezi mbalimbali ya viungo ili kujikinga na ugonjwa wa Uviko - 19.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zuwena Omary wakati wa uzinduzi wa klabu ya mazoezi ya umoja huo(UVCCM  KAHAMA JOGGING CLUB) uliofanyika katika uwanja wa halmashauri ya manispaa ya Kahama.

"Niwaombe vijana muendelee kufanya mazoezi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wetu Samia Suluhu Hasani la kuhamasisha wananchi kushiriki katika mazoezi mbalimbali ya viungo ili kukabiliana na maradhi mbalimbali,"alisema Omary

Sambamba na hilo  amewaomba wananchi bila kujali itikadi za vyama vyao  kujitokeza kwa wingi kufanya mazoezi ya mwili ili kuendelea  kuimarisha afya zao.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga amewapongeza viongozi wa  UVCCM Kahama kwa ubunifu wao kwa kuanzisha kilabu hiyo ya mazoezi itakayokuwa inawaunganisha vijana kupitia michezo.

"Ofisi yangu itashirikiana  nanyi katika hiki mlichokianzisha na tarajieni makubwa zaidi kutoka kwangu,"alisema Kiswaga.

Naye  Katibu wa UVCCM Kahama Sebastian Maganga amewashukuru viongozi hao kwa kukubali kutenga muda wao na kushiriki uzinduzi wa Klabu hiyo ya mazoezi iliyoanza kazi rasmi siku ya leo.

"Sisi kama vijana wa chama tumethubutu kuanzisha UVCCM JOGGING  CLUB ili kuwakutanisha vijana wa chama chetu kutoka majimbo ya Kahama mjini,Msalala na  Ushetu ili kuhakikisha afya zao zinaimarika,"alisema Maganga.

Zaidi ya  vijana 300 wameshiriki katika mazoezi hayo yaliyofanyika katika viunga vya uwanja wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments