TANZANIA KUPOKEA MAWAKALA WA UTALII 30

Na Magrethy Katengu  -Dar es salaam
 
KAMPUNI ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), ambayo imekuwa balozi mzuri na lango la kuingiza watalii na wawekezaji kutoka majimbo yote 50 ya Marekani inatarajia kupokea ugeni wa Mawakala wa Utalii zaidi ya 30 kutoka nchini Marekani, Ufaransa na Lithuania kuanzia Novemba 23, 2021.

 Katika ujumla wao, Mawakala wa Utalii hao zaidi ya 30 wanawakilisha maelfu ya watalii kutoka nchi zilizotajwa ambao sasa wanatarajiwa kutemebelea Tanzania.
 
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam Kaimu Mkurugenzi wa Masoko bodi ya utalii Feix John amesema mafanikio ya ujio wa mawakala hao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ilizochukua KITS baada ya kuona taarifa za Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki kutengeneza makala ya filamu ya kutangaza vivutio vya utalii duniani ijulikanayo kama “Royal Tour” ambayo kwa awamu hii imefanyika nchini Tanzania. 

Afisa uendeshaji Mkuu Kampuni ya KITS Bw. Francis Malugu, alisema kazi ya kuwataarifu Mawakala hao wa utalii kuhusu filamu hiyo ya 'Royal Tour' ilifanywa na kampuni hiyo ya KITS, yenye Makao Makuu yake jijini Washington, DC nchini Marekani na ofisi zake za uendeshaji zilizo jijini Arusha.
 
"Mara baada ya kupata taarifa mapema za utengenezaji wa makala hiyo ya filamu na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atakayekuwa muongozaji mkuu, tuliwataarifu mawakala wa Utalii katika vyama vya utalii duniani ambavyo KITS ni mwanachama wake na zaidi ya mawakala 30 waliomba na kuthibitisha kuja kuitembelea Tanzania, Novemba mwaka huu." alisema afisa huyo wa KITS, Bw. Malugu.
 
Pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia  kwa uamuzi aliouita wa busara na wa makusudi wa kuitangaza Tanzania kupitia ziara hiyo maarufu ya “Royal Tour”.

Akielezea sababu za kupongeza uamuzi huo wa Rais, Bw. Francis Malugu alisema kwamba utasaidia kuongeza nguvu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kukuza uwekezaji na kuvutia utalii kama ambavyo KITS imekuwa ikifanya nchini Marekani.

Hata hivyo amesema Bw.Francis Malugu kwa kusema kuwa kukamilika kwa makala ya filamu hiyo itasaidia kurahisisha shughuli za utangazaji utalii  ambazo kampuni ya KITS imekuwa ikizifanya katika nchi mbalimbali.

Sanjari akitaja mikutano na matukio ya kimataifa watakayoshiriki amesema  ni pamoja na Oktoba 10 hadi 11 mwaka huu nchini Ufaransa katika onesho la 'Top Resa', Travel Adventure Show itakayofanyika majiji ya Atlanta, Georgia na San Francisco, California. Tukio jingine kubwa wanalokwenda kushiriki KITS ni pamoja na National Tour Association (NTA) Annual Convention linalofanyika jijini Clevelend, Ohio ambalo litahusisha mawakala wa utalii zaidi ya 2,300 kutoka majimbo yote ya Marekani na nchini Canada.

"Ni matarajio yetu kuwa kama makala hiyo itakuwa imekamilika katikati mwa Novemba, KITS itatumia ushawishi wake kueneza kwa wateja wake juu ya kuonyeshwa kwa makala hiyo ya Rais Samia wakati wa tukio la ufunguzi wa Kongamano hilo." alisema.

Aidha kwa niaba ya Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KITS Bi. Vonnie Kiondo, Bw.Francis Malugu ametoa shukrani za dhati kwa ushirikiano ambao kampuni yao imekuwa ikipewa na mamlaka mbalimbali za serikali ukiwemo ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka za Hifadhi za TANAPA, TAWA na Ngorongoro, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC) taasisi ambazo zina dhamana ya kuendeleza utalii na wadau wakubwa katika shughuli za kuvutia uwekezaji na utalii nchini. 

Pia amesema matarajio yetu kuwa makala hii inayorekodiwa na Mh.Rais Samia itakuwa nyenzo muhimu katika shughuli za utangazaji zinazoendelea ili kuisaidia nchi kufikia lengo la watalii millioni 5 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025 licha ya kuwepo kwa changamoto za Uviko 19 zinayoikabili dunia.
 
Hata hivyo  akuzungumzia faida ya filamu hiyo anayotengeneza Rais Samia kwa sekta ya utalii, Afisa huyo Bw. Francis Malugu, alisema itasaidia kuifanya dunia kuitambua Tanzania kama sehemu mahususi ya asili ya dunia ambayo kila mpenda utalii duniani anapaswa kuitembelea. Makala hiyo ya utalii pia itachagiza na kuchochea uchumi wa nchi kupitia watalii, wawekezaji na wafanyabiashara.

Kwa niaba ya Mwenyekit na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya KITS Bi. Vonnie Kiondo, Bw. Francis Malugu alisema wao kama wadau wa sekta ya utalii wameupa uzito uamuzi huo na wanampongeza kwa moyo wa dhati Mh.Rais Samia na kuunga mkono juhudi anazozichukua za kuimarisha sekta ya utalii ikiwa ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa hapa nchini.

Pia alitoa wito kwa Serikali na Balozi wa Tanzania nchini Marekani kama itampendeza, wakati Rais Samia akifika nchini Marekani kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo itakayoanza kuoneshwa Novemba mwaka huu kutoa fursa ya kushiriki kwa watanzania wanaojihusisha na kushawishi watalii kuja nchini kutalii na kuwekeza.

Pia, akizungumzia dhamira kuu ya kampuni hiyo alisema ni kuchangia ukuaji wa uchumi kutokana na kazi wanazozifanya za kuongoza watalii, kuvutia watalii, kutoa utalaamu wa ukuzaji wa biashara hasa ya utalii kwa kutangaza vivutio vya kitalii, kutoa elimu kwa taasisi na makundi mbalimbali pamoja na kuvutia uwekezaji.

Aidha amesema jambo hilo linaweza kuwa faraja kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikihamasisha mabalozi na watanzania waishio nje ya nchi kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments