PURA YATILIA MKAZO UHAULISHAJI WA UJUZI


Mfanyakazi wa kigeni mwenye asili ya China akifanya kazi sambamba na wafanyakazi wa kitanzania katika mradi wa ufungaji wa kompresa unaotekelezwa katika Kitalu cha Songo Songo.

************************************

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) imeendelea kuhakikisha kuwa suala la uhaulishaji wa ujuzi (skills transfer) linazingatiwa ipasavyo wakati wa utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini. Kwa mujibu wa Kanuni za Ushiriki wa Wazawa (Local Content) katika sekta ndogo ya petroli za Mwaka 2017, PURA imepewa jukumu la kuhakikisha watanzania wanajengewa uwezo kupitia njia mbalimbali ikiwemo uhaulishaji wa ujuzi kutoka kwa raia wa kigeni (expatriates) wanaofanya kazi katika miradi ya mkondo wa juu wa petroli.

Katika kutelekeza jukumu la uhaulishaji wa ujuzi, PURA kupitia ziara za kaguzi maeneo ya miradi imeendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa kigeni waliobobea katika eneo husika wanafanya kazi sambamba na wafanyakazi wa kitanzania na kwamba wafanyakazi wa kitanzania hawaachwi nyuma katika kazi za kitaalamu zinazotekelezwa kwa kigezo cha kutokuwa na ujuzi wa kutosha. Ingawa uhaulishaji wa ujuzi huchukua muda na huhitaji ufuatiliaji makini, PURA imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha suala hili linatekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mathalan, katika kazi inayoendelea ya ufungaji wa mitambo ya kugandamiza gesi asilia (feed gas compression project) katika Kitalu cha Songo Songo kilichopo Mkoani Lindi, PURA imekuwa ikihakikisha kuwa kampuni ya Kichina iliyopewa kandarasi ya kutekeleza mradi huo (China Petroleum and Technology Development Co. – CPTDC) inazingatia uhaulishaji wa ujuzi kwa kutoa fursa kwa wafanyakazi wa kitanzania walioajiriwa katika mradi huo kufanya kazi sambamba na raia wa kigeni wanaotekeleza mradi.

Mradi wa ufungaji wa mitambo ya kugandamiza gesi asilia (Kompresa) unalenga kuongeza mgandamizo wa gesi itokayo kwenye visima vya uzalishaji ili kuwezesha gesi hiyo kusafiri na kufika Dar es Salaam katika mgandamizo (pressure) unaotakiwa.

Uzalishaji wa gesi asilia kutoka kwenye Kitalu cha Songo Songo ulianza mwaka 2004 ambapo mpaka kufikia Juni, 2021 kiasi cha futi za ujazo 469.13 Bilioni kilikuwa kimezalishwa kwa matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments