MTOTO AFARIKI DUNIA BAADA YA KUSHAMBULIWA NA FISI

 

Mnyama fisi

Na Costantine Mathias, Maswa

Mtoto  mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Zawa, Kata ya Sengerema wilayani Maswa mkoani Simiyu amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na fisi huku baadhi ya viungo vyake vya mwili vikiliwa na mnyama huyo.

Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi Richard Abwao wakati akiongea na waandishi wa habari ofisi kwake ambapo alisema mtoto huyo alijeruhiwa wakati akichunga mifugo na watoto wenzake.

 Alisema mnamo tarehe 08/09/021 majira ya 15:00 huko katika kitongoji cha Mwang’honori, kijiji cha Zawa,Tarafa ya Sengerema, Wilaya ya Maswa na Mkoa wa Simiyu, Masule Cosmas  (05) mtoto, mkazi wa Mwang’honori, alifariki baada ya kujeruhiwa na mnyama mkali fisi na baadhi ya viungo vya mwili wake kuliwa.

"Tukio hilo limetokea wakati akiwa na wenzake ambao ni Naomi Amos na Scolastika Wahumija, wakiwa wanachunga Ng'ombe na Mbuzi  kwenye mashamba ambayo yapo umbali kidogo na makazi yao", alisema


"Fisi huyo alitokea kwenye kichaka na kuanza kuwakimbiza na alifanikiwa kumkamata na kuanza kula baadhi ya viungo vya mwili wa Masule Cosmas ambavyo ni shavu la kulia na kumtoa ngozi ya kichwa pamoja na macho yote mawili’’ alieleza Kamanda Abwao.

Katika taarifa yake, Kamanda Abwao alifafanua kuwa wananchi wa eneo hilo walimtafuta fisi huyo na baada ya kumpata walimuua ambapo mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na Daktari na baadaye kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la polisi mkoa wa Simiyu, linatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto pamoja na wazazi wao dhidi ya wanyama wakali kwenye maeneo yao, hasa vijijini pia kuwaepusha watoto kutembea pekee yao kwenye maeneo yasiyokuwa na makazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments