LHRC : NI WAKATI MUAFAKA WA NCHI YA TANZANIA KUWEKA MABORESHO YA MFUMO WA DHAMANA

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu Anna Henga 

Na Jackline Lolah Minja  -Morogoro
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu Anna Henga amesema ni wakati muafaka wa nchi ya Tanzania kuweka maboresho ya mfumo wa dhamana kutokana na kwamba mfumo uliopo unaweza kutumika kwa lengo baya la kuumiza mtu kisaikologia na kimwili.

Ameyasema hayo leo Septemba 6 2021 wakati akifungua  kikao kazi na wadau kwaajili ya kutoa wasilisho la ripoti ya makosa yasiyo na dhamana ambapo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) iliangalia mfumo wa utoaji haki ya dhamana wa hapa nchini kwa kipindi cha mwaka 1945 hadi 2021 kuwa sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1945 iliipa mamlaka mahakama kuu kusikiliza maombi ya dhamana hata katika makosa yasiyo na dhamana.

"Sheria hii ilidhihirisha kwa vitendo dhamana ya uhuru pamoja na dhana yakutokuwa na hatia hadi pale mahakama itakapothibitisha hivyo katika kipindi cha kuanzia mwaka 1945 hadi 1984  mahakama kuu ilikuwa na uwezo huo katika makosa yasiyo na dhamana , kwa bahati mbaya sheria na mwenendo wa makosa ya jinai 1985 iliondoa kifungu kilichoipa mahakama mamlaka hiyo hivyo kwa sasa mtu atakaye tuhumiwa na kosa lisilo na dhamana uhuru wake unapokonywa mpaka kesi yake itakapo hitimishwa na mahakama", amesema Anna Henga

Aidha Henga amesema utafiti huu ulifanya ulinganifu wa mfumo wa utoaji haki katika makosa ya aina hiyo katika nchi tano (5) za Kenya , Uganda,  Malawi , Zambia na Zanzibar.

"Niseme tu kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika mifumo ya nchi za jirani ili kuboresha mfumo wetu na ni imani yetu kwamba mkutano huu utachochea mabadiliko na hoja zenye uzito baada ya kupata mwanga wa kufahamu kwa kina kutoka wasilisho la leo", amesema Henga. 

Henga ameongeza kuwa  mchakato wa upatikanaji haki kupitia mfumo uliopo sasa wa haki ya jinai unapingana na dhana iliyopo nchini ya ibara ya 13 (6)b ya katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoweka dhana ya msingi ya kutokuwa na hatia hadi mahakama itakapothibitisha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments