KOREA KASKAZINI YAZIONYA MAREKANI, UINGEREZA NA AUSTRALIA KUHUSU MAKUBALIANO YAO YA NYAMBIZI YA NYUKLIA

Korea Kaskazini imesema makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya nchi tatu za Marekani, Uingereza na Australia ni hatua hatari sana.

Kufuatia uamuzi uliofikiwa na Marekani na Uingereza wa kuipatia Australia nyambizi ya nyuklia, serikali ya Pyongyang imetangaza leo kuwa, hatua hiyo ni mwanzo wa kuibuka mashindano ya uundaji silaha za nyuklia.

Duru za Pyongyang zimeripoti kuwa, Korea Kaskazini inaendelea kuchunguza athari na matokeo ya uamuzi huo wa Marekani na Uingereza ili kuweza kuchukua hatua mwafaka pale itakapolazimu kufanya hivyo.

Kabla ya msimamo huo uliotangazwa na Korea Kaskazini, China, Russia na Indonesia, nazo pia zilitamka kuwa, hatua hiyo iliyochukuliwa hivi karibuni na Marekani, Uingereza na Australia inatia wasiwasi na itavuruga mlingano wa kiusalama katika eneo.

Jumatano, tarehe 15 Septemba, maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon walisaini makubaliano na wenzao wa Uingereza ya kuipatia Australia nyambizi ya nyuklia, hatua ambayo imezikasirisha nchi nyingi duniani ikiwemo Ufaransa.

Katika kulalamikia makubaliano hayo, ambayo yamesababisha kufutwa mkataba uliosainiwa kati ya Ufaransa na Australia, ambapo Ufaransa ingeiuzia Australia nyambizi zenye thamani ya dola bilioni 66, Paris imechukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa, ya kuwaita nyumbani mabalozi wake wa Washington na Canberra.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments