FREEMAN MBOWE NA WENZAKE WASOMEWA MASHTAKA UPYA


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamesomewa upya mashtaka yao sita mbele ya Jaji Mustapher Siyani.

Mbowe na wenzake wamefikishwa katika Mahakama hiyo mapema asubuhi ya leo wakiwa chini wa ulinzi mkali wa Jeshi la Magereza pamoja na Polisi.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling’wenya.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo, wamekana kutenda makosa yote.

Washtakiwa baada ya kukana mashtaka yao, kiongozi wa jopo la upande mashtaka wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando ameiomba mahakama hiyo iruhusu washtakiwa wasomewe maelezo ya awali.

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo ya awali namna wanavyodaiwa kutenda makosa yao na wakili wa Serikali, Tulimanywa Majingo.

Baada ya kusomewa maelezo hayo washtakiwa wamekubali taarifa zao binafsi na wamekana mashtaka yote.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa wamesomewa idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka ambao ni 24 na vielelezo zaidi ya 19.

Kwa upande wa utetezi, Wakili Peter Kibatala amesema wanatarajia kuwa na mashahidi 11, wakiwemo washtakiwa wenyewe, huku mashahidi wanne Kati ya hao, akiomba Mahakama asiwataje majina yao na anuani zao kwa sababu za kiusalama.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makosa ambayo wnadaiwa kuyatenda kati ya Agosti Mosi na 5 mwaka 2020 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Morogoro, Moshi na Dar es Salam.

Katika kesi hiyo Mwenyekiti huyo wa CHADEMA anatetewa na Wakili Peter Kibatala akisaidiana na jopo la Mawakili wa kujitegemea.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments