Na Marco Maduhu, Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, amewataka wafanyabiashara wa kuuza mbao, ambao bado wapo kwenye Soko la Kambarage Manispaa ya Shinyanga, wahamie mara moja kwenye eneo ambalo wametengewa na Serikali lililopo Chamaguha, kabla ya kuwachukulia hatua.
Mboneko alibainisha hayo jana, alipofanya ziara ya kutembelea kwenye eneo jipya la kuuza mbao lililopo Chamaguha na kupewa malalamiko kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara bado hawajahamia huko na kubaki Kambarage na kuombwa awaondoe ili wafanye biashara eneo moja.
Alisema Serikali iliwaondoa wafanyabiashara kwenye soko hilo la Kambarage, ambalo lilikuwa finyu na siyo rafiki kwao kufanyabiashara hiyo ya kuuza Mbao, na kuwatengea eneo zuri la Chamaguha, na kuwataka wale ambao bado wapo Kambarage watii maagizo ya Serikali na kuhamia kwenye eneo hilo jipya.
“Naagiza wale wafanyabiashara wa mbao ambao bado wapo huko Kambarage, waondoke mara moja, waje huku Chamaguha kwenye eneo lao, watii maagizo ya Serikali,”alisema Mboneko.
Pia, aliwataka akina mama kuchangamkia fursa ya kuuza chakula kwenye eneo hilo jipya la kuuza mbao Chamaguha, ili wajipatie kipato na kuendesha maisha yao.
Nao baadhi ya wafanyabiashara hao wa kuuza mbao ambao wamehamia kwenye eneo hilo jipya, walisema wanasikitika kuona wenzao bado wapo huko Kambarage wakifanya biashara, na kugoma kuhamia Chamaguha kwenye eneo ambalo limetengwa na Serikali kwa ajili ya biashara hiyo, na kumuomba Mkuu huyo wa wilaya awaondoe huko.
Na Marco Maduhu- Shinyanga
No comments:
Post a Comment