TWCC YAPOKELEWA KWA SHANGWE SINGIDA


Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Dorothy Mwaluko akikagua bidhaa za wajasiliamali wanawake mkoani hapa kabla ya kuzindua mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kuinua ubora wa bidhaa wanazozalisha yaliyoandaliwa na Chama Cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC)
Viongozi wapya wa chama cha wafanyabiashara wanawake walio chaguliwa hivi karibuni mkoa wa Singida.
Wajasiliamali kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Singida na baadhi ya wawezeshaji mbalimbali kwenye mafunzo hayo ya TWCC wakifuatilia matukio yanayoendelea
Mmoja wa wajasiliamali wanawake akipokea cheti cha ushiriki wa mafunzo hayo.
Picha ya pamoja ya wafanyabiashara wanawake, wawezeshaji na viongozi mbalimbali wakati wa mafunzo hayo mkoani Singida.


***
Na Edina Malekela, Singida

Chama Cha Wafanya Biashara Wanawake Tanzania (TWCC) kimeshauri kuanzishwa kwa kituo cha pamoja cha utoaji wa huduma kwa wajasiriamali wanawake (One Stop Centre) ili kuwawezesha kupata wepesi kwenye upatikanaji wa huduma zao.

Aidha chama hicho kimeshauri taasisi zote zinazohusika katika utoaji wa mafunzo na maelekezo mbalimbali ya namna bora ya ufanyaji biashara zihakikishe zinashuka mpaka chini ili kutoa elimu stahiki kwa lengo la kutosheleza taarifa husika.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa TWCC Taifa, Mercy Sila wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali Mkoani Singida jana.

"Ifike mahali kuwe na One Stop Centre ambayo itatoa package ya wao kuwezeshwa zaidi kwenye eneo la mazingira ili wajiamini, wafanye na wasimame wenyewe kiuchumi," alisema Sila.

Alisema wanawake wengi wanania njema ya kuwekeza na kutaka kujinyanyua kiuchumi lakini wanakosa taarifa nyingi za kufanikisha ndoto zao kutokana na taasisi nyingi zinazopaswa kuwahudumia kutofanya hivyo kwa wakati.

Sila katika hatua nyingine aliwasihi wanawake wajasiriamali kujikita katika kusikiliza, kutambua, kuelewa , kujidhatiti na kuthubutu ili kusonga mbele kiuchumi.

Aidha alishauri kwa mwanamke yeyote anayetaka kufanikiwa kwa haraka kwenye ujasirimali hapaswi kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja bali vichache ambavyo anaona ataweza kuwekeza nguvu yake sambamba na kufuata taratibu stahiki za biashara husika ili kunyanyuka kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza alisema mafunzo hayo ambayo yameshirikisha wilaya zote za Mkoa wa Singida yamelenga kuelimisha juu ya masuala ya viwango, uzalisha ubora wa bidhaa kwa kuzingatia kanuni za uzalishaji bora ili kuwawezesha wajasiliamali kushindana kwenye soko.

Mwajuma alisema kikubwa walichokibaini kupitia mafunzo hayo ambayo yalikita katika usalama wa vyakula, vipodozi na sabuni ni kwamba idadi kubwa ya wajasilimali bado wanazalisha bidhaa ambazo hazikidhi viwango.

"Mapungufu yaliyopo moja ni wengi bidhaa zao hazina TBS , hazina Barcode lakini wengi pia hawajui aina bora ya vifungashio kwa aina ya bidhaa wanazozalisha....Pia asilimia 95 ya lebo hazikidhi viwango na zaidi kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa vifungashio," alisema Mkurugenzi Mtendaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments