SERIKALI YAUNDA TIMU MAALUMU YA KUPITIA MFUMO WA MAUZO YA MAZAO YA DENGU, CHOROKO,MBAAZI NA UFUTA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda  akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
 
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Serikali imeunda Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta kwa ajili ya kusikiliza na kupokea maoni kwa wadau kuhusu namna bora ya kutekeleza ununuzi wa mazao hayo katika mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao umeleta mivutano ya hapa na pale kama vile kuzuia na kuachia mazao ya dengu yaliyokuwa yanasafirishwa na wafanyabiashara.

Timu hiyo imetangazwa leo Jumatano Septemba 15,2021 na Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.


“Tumekuwa na kikao kizuri sana na Uongozi wa Mkoa wa Shinyanga. Mtakumbuka hivi karibuni mkoa wa Shinyanga ulikuwa unatekeleza Mwongozo wa Stakabadhi ghalani lakini kutokana na changamoto iliyojitokeza, tulizungumza na Mkoa tukawaomba tusitishe stakabadhi ghalani kwanza ili tuangalie ni mambo gani tuyaweke sawa ili utaratibu huu ufanyike bila kuwa bughudha ama kwa mkulima au mfanyabiashara au mtu mwingine yeyote”,amesema Prof. Mkenda.

“Napenda kumshukuru Mkuu wa Mkoa kuwa baada ya mazungumzo walisitisha utaratibu huo na tulikubaliana kuwa tutakuwa na Timu ambayo itapita na kusikiliza maoni ya sehemu mbalimbali kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja na vile vile mapendekezo ya namna bora ya kutekeleza stakabadhi ghalani”,ameeleza.

“Kwa hiyo leo tumekuja na Timu ya kupitia mfumo wa mauzo ya mazao ya dengu, choroko, mbaazi na ufuta na hatua gani inatakiwa tuchukue ili utaratibu wa stakabadhi ghalani ukitumika usiwe na bughudha. Hivyo napenda kuitambulisha timu hii ambayo itapitia kila kitu katika mkoa wa Shinyanga, Morogoro na Lindi katika kipindi cha mwezi mmoja na matokeo yatakayopatikana tutayatangaza”,ameongeza Prof. Mkenda.


Prof. Mkenda amesema Timu hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Dkt. Hamis Mwinyimvua aliyekuwa Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Katibu Bw. Ernest Doriye kutoka Wizara ya Kilimo na wajumbe ambao ni Dkt. Anaclet Kashuliza kutoka SUA, Dkt. Ruhinduka Remidius kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Bw. Barney Laseko kutoka Sekta Binafsi na Dkt. Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na Wajumbe wa Sekretariati ambao ni Shaibu Chilavi na Samson Poneja.

Amesema kupitia Timu hiyo wadau ambao wana maoni kuhusu namna bora ya kufanya stakabadhi ghalani wataweza kutuma maoni yao na kwamba timu hiyo itakuwa na jukumu la kutengeneza vigezo gani vitumike kuamua zao flani liingie katika mfumo wa stakabadhi ghalani na utaratibu gani utumike kwa wakulima kupata fedha kabla ya mauzo halisi hayajafanyika.

“Tukumbuke Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati anahitimisha Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema mwelekeo wetu ni kuelekea stakabadhi ghalani lakini alielekeza Wizara ya Kilimo itengeneze mazingira mazuri ili stakabadhi ghalani itakapokuwa inafanya kazi isiwe na bughudha kwa mtu yeyote, kwa hiyo hii ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu”, ameongeza Prof. Mkenda.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta, Dkt. Hamis Mwinyimvua amesema katika utekelezaji wa kazi yao watakahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanya biashara, viongozi wa serikali na vyama vya ushirika.

“Maoni ya wadau ni muhimu sana katika kuboresha yale ambayo tunayategemea. Tutashauri wapi parekebishwe. Kwa wale ambao hawataweza kutufikia basi wanaweza kutupigia simu namba 0784 471838”,amesema Mwenyekiti wa Timu hiyo.

Naye Mkuu wa Mko wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameahidi viongozi wa mkoa watatoa ushirikiano mkubwa kwa timu hiyo ili kupata taarifa za msingi kuhusu maendeleo na changamoto ya mfumo wa manunuzi ya mazao jamii ya kunde ili waweke mapendekezo yatakayosaidia kuwa na msimamo wa pamoja ambao ni endelevu juu ya mfumo wa Stakabadhi ghalani.

“Sisi viongozi wa Mkoa wa Shinyanga tumefarijika sana kwa ujio wako Mhe. Waziri wa Kilimo pamoja na Timu hii kwa sababu tunataka kufanya kazi pamoja kama timu kwa sababu serikali ni moja na tunataka twende pamoja katika masuala ya msingi kwenye ustawi na maendeleo ya taifa letu. Na eneo ambalo tunatakiwa tufanye kazi kwa upendo kama timu ni eneo la kilimo. Tunashukuru Mungu sintofahamu iliyokuwepo kuhusu ununuzi wa mazao jamii ya mikunde imeisha”,ameongeza Dkt. Sengati.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda  akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda  akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
Mwenyekiti wa Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta, Dkt. Hamis Mwinyimvua akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
Mwenyekiti wa Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta, Dkt. Hamis Mwinyimvua akizungumza katika mkutano wa Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021.
Mkutano wa Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 15,2021 ukiendelea.

Picha na Marco Maduhu na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments