POLISI ARUSHA WAKAMATA SILAHA AK - 47 ILIYOTELEKEZWA NA MTUHUMIWA MATUKIO YA UHALIFU - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Wednesday, September 15, 2021

POLISI ARUSHA WAKAMATA SILAHA AK - 47 ILIYOTELEKEZWA NA MTUHUMIWA MATUKIO YA UHALIFU

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha

Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha lilifanikiwa kupata silaha moja aina ya AK 47 ambayo iliyotelekezwa na John Ghakwa Kepteni  anayetuhumiwa kufanya matukio mbalimbali kihalifu katika maeneo hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP  Justine Masejo amesema tukio hilo limetokea Septemba 14, 2021 muda wa saa 12:20 jioni  katika kijiji cha Jema kata ya Oldonyosambu wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

"Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha lilifanikiwa kupata silaha moja aina ya AK 47 ambayo ilitelekezwa na mtuhumiwa John Ghakwa Kepteni mkazi wa kijiji cha Jema ambaye anatuhumiwa kufanya matukio mbalimbali kihalifu katika maeneo hayo",amesema Kamanda Masejo.

"Taarifa za awali zinaonesha kwamba, mtuhumiwa huyo kipindi cha nyuma alishiriki katika matukio kadhaa ya uhalifu ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na kujihusisha na Ujangili katika Mbuga za Wanyama zilizopo nchini kisha kufanikiwa kukimbilia nchi jirani lakini hivi karibuni kupitia idara yetu ya intelijensia ilipokea taarifa juu ya uwepo wake hapa nchini",ameeleza.

Amesema kuwa baada ya taarifa hiyo walianza kumfuatilia ambapo Septemba 14, 2021 muda wa Jioni askari Polisi walifanikiwa kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na  kuizingira nyumba anayoishi mtuhumiwa huyo ambapo baada ya kufika eneo hilo walifanya upekuzi lakini  hawakuweza kumkuta mtuhumiwa ila walifanikiwa kupata silaha hiyo ya kivita aina ya AK 47 isiyokuwa na namba ikiwa na risasi 10 ndani ya Magazine.

Kamanda Masejo ameendelea kusema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo pamoja na mtandao wake na pindi atakapopatikana atafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili. 

Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kudumisha hali ya usalama katika mkoa wetu.

Pia  amewaonya vikali wahalifu kuwa  Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha halitowafumbia macho wahalifu wenye nia ya kuharibu na kuvuruga rasilimali za nchi pamoja na hifadhi za taifa.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

No comments:

Post a Comment

Pages